Na WAF- DODOMA.
KATIBU MKUU Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amewaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa Chanjo nchini kuimarisha utoaji elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya magonjwa.
Prof. Makubi amesema hayo leo Februari 1, 2023 wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya kampeni ya Chanjo ya polio awamu ya nne kilicho hudhuriwa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa chanjo pamoja na Wadau mbalimbali katika Sekta ya afya.
“Niendelee kutoa wito kwenu nyote kutoa elimu kwa wananchi wote na kuwajuza juu ya umuhimu wa chanjo ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko.” Amesema Prof. Makubi.
Sambamba na hilo Prof. Makubi amewaagiza wataalam hao kwenda kusimamia uchanjaji wa chanjo ya Polio na kuhakikisha huduma za chanjo kwa njia ya mkoba zinafanyika na kuwafikia watoto wote ambao hawajapata au kukamilisha ratiba ya chanjo.
Aidha, Prof. Makubi amewataka kuhakikisha wakati wanapopambana kuongeza uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19 huduma zingine za Afya ikiwemo chanjo za watoto ziendelee kutolewa vyema ili kutoruhusu milipuko ya magonjwa mengine hasa yaliyokwisha kupunguzwa au kutokomezwa.
Pia, amesema, Ili tuweze kuzuia ongezeko la wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ni vyema kuweka mikakati ya kuongeza kiwango cha uchanjaji wa chanjo hii kupitia vikao vya usimamizi wa huduma za Afya vya Mikoa na Halmashauri ili kufikia mwisho wa mwaka 2023 kila mkoa uweze kuvuka lengo la asilimia 95 ya uchanjaji wa chanjo hii na chanjo zingine zote.
Pamoja na hayo, Prof. Makubi amewataka Wataalamu wote kujikita katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote itayomsaidia kila mwananchi kupata matibabu bila malipo kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka hospitali ya Taifa.
Lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuhakiksha kila mwananchi anapata huduma bora na salama pasipo usumbufu, ujio wa bima ya Afya kwa wote utaweza kusaidia kuwa na huduma endelevu zikiwemo za chanjo zisizotegemea wadau katika uendeshaji wake pindi watakapo sitisha ufadhili wao. Amesisitiza Prof. Makubi.
Akitoa salamu kwa niaba ya Waganga wakuu na Waratibu wa Chanjo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Best Magoma amesema, jitihada kubwa za utoaji chanjo kwa wananchi tayari zimefanywa na zimesaidia kuwakinga wananchi kwa kiasi kikubwa.