Taasisi ya wakurugenzi Tanzania (IODT) imetoa mafunzo kwa watu zaidi ya 100 ambao ni wakurugenzi kutoka taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kuhusiana na suala zima la uongozi ili kuweza kuwajengea uwezo.
Akiongea na waandishi wa habari mkurugenzi wa taasisi hiyo Said Baraka Kambi alisema kuwa uongozi ni mojawapo ya mambo yanayoendana na kukua ndani ya maisha na mara nyingi huwezi kupata yakiwa yanafundishwa kwasababu ni tofauti na mafunzo ambayo yana msingi wa ufahamu wa masomo yanayotokana na kubadilisha tabia.
“Tuna mafunzo mengi lakini pia tunafanya kazi za ushauri na haya mafunzo ambayo tunayafanya Arusha kwa hizi siku tano ni mafunzo yetu ambayo yanakuwa kwenye kalenda ya mwaka na haya ndio ya kwanza kwa mwaka 2022 ambayo leo tumeanza na cheti cha ukurugenzi ambapo katika mashirika na tasisi ukurugenzi ndio uongozi mkubwa zaidi,” Alieleza.
“Na baada ya cheti wanapata uzoefu zaidi ambapo kesho tutaanza rasmi kozi ya upeo katika ukurugenzi lakini pia kozi ya ukatibu katika mabodi na mabaraza ambayo pia ni kazi muhimu ya msingi kwasababu katibu ndio mwenezi na ambaye ndiye anaweza kuchukua taarifa na kupangilia mambo,”Alisema Kambi.
Alieleza kuwa wana watu zaidi ya 60 kwenye darasa la cheti lakini pia watu zaidi ya 30 kwenye darasa la upeo na watu 15 kwenye darasa la ukatibu ambapo kwa mwaka huu wa 2022 ni mwaka wa kumi tangu kuanza kutoa mafunzo hayo na mwitikio wa watu kushiriki ni mzuri kwani mashirika ambayo yamekuwa yakipeleka watu kujifunza yamekuwa yakiendelea kufanya vizuri.
“Viongozi wetu wanakuwa zaidi na zaidi na wengine wamekuwa wakionekana katika nafasi za juu za serikali pamoja na taasisi za umma hivyo tungependa kuwakaribisha watu kwenye tovuti yetu kujua taarifa lakini pia kujiunga na mafunzo hasa vijana wadogo ambao bado itawachukua muda sana kwa uzoefu kuweza kujifunza uongozi ambapo hapa watapata uwezo wa mara moja,” Alisema.
Kwa upande wake Kanali mstaafu Joseph Leon ambaye ni mwezeshaji katika mafunzo hayo alisema kuwa nchi imefungua mipaka ambapo makampuni mbalimbali yanakuja kuwekeza na watanzania wanahitajika kushiriki na kusipikuwepo na watu wenye elimu, maarifa, na uwezo wa kuwa viongozi watabaki kulalamika viongozi wakuu katika mashirika hayo ni kwanini lazima watoke nje na sio watanzania.
“Tunaweza kusema kuwa mbona tuna watu wanatoka chuo kikuu lakini hiyo haitoshi kwani hiyo ni elimu ya msingi lakini ule uongozi wa kufanya kibiashara una vigezo vyake na maarifa yake ya kimataifa na ndicho tunachokifanya hapa ili kuweza kuwa na kada ya viongozi watakaoweza kuongeza makampuni ya kibiashara na tasisi zingine zote zikiwemo zinazohisiana na masuala ya kiuchumi,” Alisema Kanali Mstaafu Joseph.
Alieleza ni muhimu kwani kwenye soko la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla kutakuwa na makampuni, mashirika na taasisi ambazo zitafanya kazi kwenye nchi zaidi ya moja ambapo mafunzo hayo yatawafanya na watanzania na wenyewe waweze kushiriki kwani ni kama daraja la kufanya watambulike.
Poniwoa Andrew Mbise independent director wa China Dasheng bank alisema kuwa mafunzo hayo ni yamuhimu kwani kuna vitu mbalimbali wanatakiwa kuvifahamu Kama viongozi ili kwenda sawa na Dunia inavyoenda kutokana na Dunia kuwa inabadilika mara kwa mara na kuna mambo mengi ambayo wanakutana nayo na mafunzo hayo yanawasaidia kuwa endelevu katika taasisi zao.
Naye meneja wa mafunzo kutoka taasisi ya wakurugenzi Tanzania Abduel Kelakela alieleza kuwa mafunzo hayo ni kwaajili ya kuwaandaa kuwa viongozi bora katika mashiraika yao na hasa katika mabodi kwasababu ndio chombo cha juu katika kufanya maamuzi kwenye mashirika hivyo ni muhimu viongozi hao wawe wamepatiwa mafunzo ya kutosha yanahusiana na utawala bora na uongozi.