Mwandishi wetu
BONDIA Mtanzania Tony Rashid amepeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kumtwanga mpinzani wake Bondia Bongani Wonder Boy Mahlangu kutoka Afrika Kusini na kuondoka na Ubingwa wa Afrika (ABU).
Mchezo huo ulitanguliwa na mapambano 10 ambayo yalianza kuchezwa Februari 25, 2022 na kupelekea mchezo uliosubiriwa na maelfu ya Watanzania kuanza kuchezwa saa 6:35 hadi saa 7:07 usiku wa kuamkia Februari 26, 2022 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na mamia ya Watanzania wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Othuman Yakubu.
Katika mahojiano maalum na waandishi wa habari, mara baada ya kumkabidhi bondia Tony Rashid mkanda wa bingwa huo, Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu amesema Serikali ipo bega kwa bega na vijana ambao wanatumia muda wao kutetea taifa lao katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Micheo ikizingatiwa ndiyo sekta ambazo zinatoa fursa za ajira kwa vijana wengi nchini.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku kila bondia akitumia nafasi kuonesha makali yake muda wote wa pambano hali iliyopelekea miamba hiyo ya mchezo wa ngumi kucheza mizunguko yote 12 ya pambano hilo ambapo Tony Rashisi amefanikiwa kumvua ubingwa huo mpinzani wake Bondia Bongani Mahlangu ambaye alikuwa akiutetea ubingwa huo wa uzani wa super bantam.
Akizungumza mara baada ya pambano hilo, Tony Rashid amewashukuru watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo, hali iliyompa nguvu, hamasa na morali iliyopelekea kupata ushindi huo na kuchukua mkanda wa ABU ambayo ni heshima kwa nchi inayojali michezo ambayo inaendelea kuiheshimisha Tanzania kimataifa.
Naye Bondia Hassan Mwakinyo ambaye alikuwa mstari wa mbele kumsimamia bingwa huyo, amesema kuwa Bondia Tony ni mtanzania ambaye amepigana pambano gumu zaidi kuliko mabondia wote nchini na kusisitiza haikuwa kazi rahisi kupata ubingwa huo.
Mabondia hawa wamekutana mara mbili ambapo katika pambano la awali Septemba 11, 2021 mchezo ambao ulichezwa jijini Dar es salaam Bondia Tony Rashid alipoteza ubingwa mchezo huo katika mzunguko wa 12 na mpinzani wake kutoka Afrika Kusini Bondia Bongani Wonder Boy Mahlangu na kuondoka na mkanda wa Ubingwa wa Afrika (ABU).