Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka wadau wa utalii nchini kuutangaza mlima Kilimanjaro hasa kipindi cha mashindano ya mbio za Kilimarathon kwa kuweka utaratibu wa kuupanda mlima huo.
Amesema hayo leo, wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Kilimanjaro Marathon 2022 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
“Natoa rai kwa washiriki wa mbio za Kili Marathon kujiwekea utaratibu wa kupanda mlima kwa matembezi ya siku ili kutumia fursa hii kujionea vivutio vya mlima wetu pamoja na kufanya maandalizi ya kushiriki mbio hizi muhimu” Mhe. Masanja amefafanua.
Amesema kuwa mbio hizo ni muhimu katika kujenga afya zetu, upendo, umoja, amani, mshikamano na kukuza uchumi mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewakumbusha watanzania kutembelea vivutio vya utalii nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kudhihirisha uzalendo.
Mbio za Kili Marathon zimetimiza miaka 20 tangu zilipoanzishwa mwaka 2002.