Na Dotto Mwaibale, Ikungi Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ameviagiza vyombo vya dola wilayani Ikungi kuchunguza matukio ya uhalifu yanayodaiwa kuhusisha watoto wenye umri usio zidi miaka 15.
Serukamba alitoa agizo hilo Januari 19, 2023 baada ya kuibuliwa na wananchi wa Kijiji cha Puma wilayani Ikungi katika mkutano wa hadhara ikiwa ni muendelezo wa ziara za kutembelea kila wilaya kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi.
Kero hiyo iliibuliwa na mwananchi wa kijiji hicho Joramu Zakaria ambaye alisema vitendo hivyo vya uhalifu vimekithiri katika eneo hilo kwa kiwango cha mtu kutokuwa na uhakika wa kuamka salama.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Samwel Mbiaji alikiri kuwepo vitendo hivyo na kuwa walifanya msako kwa kushirikiana na polisi na kuwa asilimia 75 ya waliokamatwa walikuwa na umri umri usiozidi miaka 15 ambao waliachiwa.
“Tukiwaita wazazi wao wanatuambia tufanye tunavyotaka wao wamewashinda sasa mkuu sisi tufanyeje” alisema Mbiaji.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ikungi, Suzana Kidiku aliahidi kulishughulikia suala hilo kwa kuwashirikisha maafisa wa ustawi, viongozi wa kijiji na kuwa wanatarajia kufanya msako wa kuwabaini wahalifu hao.
Kero nyingine iliyoibuliwa katika mkutano huo ni ile iliyotolewa mfanyabiashara wa viazi Fatuma Ramadhani ambaye aliomba kuwepo kwa soko la uhakika kwa kuwa hivi sasa wanauza bidhaa hiyo maeneo yasiyo rasmi na kusababisha kuchafua mazingira.
Pia alilalamikia utozwaji wa ushuru mara mbili unaofanyika eneo la Kintinku baada ya kutozwa wa awali wanapotoka katika kijiji hicho.
Kufuatia kero hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alisema wanatarajia kujenga soko la kisasa katika kijiji hicho ambalo litaondoa changamoto hiyo.
Akizungumza baadaya kupokea kero hizo Serukamba amewataka viongozi na watumishi wa Serikali wilayani humo kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii ya kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema jambo kubwa aliloliona baada ya kusililiza kero hizo ni baadhi ya viongozi kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na akawaomba viongozi hao kwenda katika Tarafa na Kata kufanya kazi hiyo na kuacha tabia ya kukaa ofisini.Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi (OCD), Suzana Kidiku akipiga saluti kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (Aliye kaa meza kuu kushoto) ikiwa ni kuonesha utii baada ya kutakiwa kushughulikia madai ya watoto kuhusishwa na vitendo vya uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akisisitiza jambo kwenye mkutano huo. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto.