Na: Abby Nkungu, Singida.
JUHUDI za Asasi za kiraia kutokomeza vitendo vya ukeketaji mkoani Singida huenda zikazaa matunda hivi karibuni baada ya kufanikiwa kubaini mbinu mpya zinazotumiwa na baadhi ya wazazi na walezi kuwasugua sehemu za siri watoto wao wachanga wa kike kwa kutumia ndulele, majivu au kuwafinya kwa kucha.
Mradi wa kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia; ikiwemo ukeketaji, unaotekelezwa na mashirika ya Action Aid na MEDO mkoani Singida umebaini kuwa baada ya Serikali na wadau wake kusimamia ipasavyo sheria ya kuzuia vitendo hivyo, wazazi na walezi wamebuni mbinu mpya za kuwafanyia mila hiyo potofu watoto wao wachanga wa kike kabla hawajajitambua.
Hayo yalibainika katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kijota Singida Vijijini chini ya mashirika hayo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya miaka mitano 2021/22 – 2025/26.
Katika mkutano huo, baadhi ya wazazi Doricas Manase mkazi wa Ilongero, Singida na Rahel Nkindwa mkazi wa Nduu walisema licha ya juhudi kubwa za Serikali na wadau wake kupinga ukeketaji, wanaoendeleza mila hiyo wamekuja na mbinu mpya kukwepa mkono wa sheria.
“Hili jambo sasa linafanyika kwa siri kubwa, mama akikaribia kujifungua anaomba ruhusa kwenda kwa shangazi yake na akishajifungua mtoto wa kike wanakifinya kwa ukucha kichanga hicho sehemu zake za siri hadi damu itoke na wakati mwingine wanamsugua kwa majivu au ndulele” alieleza Doricas.
Naye Rahel alisema ukatili huo sasa unafanyika bila wanaume kujua kwani wengi wao wameelimika; hivyo akaomba Serikali kutoa kibali cha watoto wote wa kike kukaguliwa na waatalamu wa afya waendapo kliniki na wataobainika kukeketwa, wazazi au walezi wao wachukuliwe hatua kali.
Afisa Muuguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Singida, Neema Mlowe alipendekeza kuwa pamoja na kuchukua hatua za kisheria ni vyema jamii ikaendelea kuelimishwa juu ya madhara ya ukeketaji.
“Hii mila pamoja na kuwa kinyume cha sheria na kukiuka misingi ya haki za binadamu, kiafya pia ina madhara kwani mwanamke aliyekeketwa huvuja damu nyingi wakati wa kujifungua na hata kupoteza maisha” alifafanua.
Hata hivyo, Naibu Mkuu wa Kituo kikuu cha Polisi Singida Inspekta Athumani Muna alisema pamoja na ukeketaji kuendelea, juhudi za mashirika hayo zimesaidia kubaini mbinu mpya za wazazi na walezi hivyo kuwa rahisi kwa mpango huo kuzaa matunda ya kukomesha vitendo hivyo.
“Tumeshajua mbinu yenu na sisi kama Jeshi la Polisi na dawati la jinsia tunaenda kujipanga upya na kuja na mbinu yetu. Lazima tushirikiane wadau wote kutokomeza mila hii potofu ambayo pia ni ukatili wa hali ya juu kwa watoto” alisema Insepkta Athumani.
Takwimu za idara ya afya mkoani Singida zinaonesha kuwa wastani wa asilimia 20 ya wanawake wanaokwenda kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wamekeketwa, wakati ripoti ya hali ya ukeketaji nchini ikionesha mkoa wa Singida unashika nafasi ya tano ukitanguliwa na Manyara, Dodoma, Arusha na Mara.
Programu Jumuishi ya Taifa ya alezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) imekuja kama mwarobaini wa kuhakikisha vitendo kama hivyo vinadhibitiwa kwa watoto walio umri wa miaka 0 hadi 8 kwa kushirikisha sekta mbalimbali ili kuleta ulinzi na usalama kwa kundi hilo muhimu.