Mratibu wa Bima za mazao na Mifugo |
Na: Hughes dugilo, MBEYA.
Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeendelea kutoa elimu ya huduma za Bima mbalimbali wanazozitoa katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Wananchi wengi wanaotembelea katika Banda la NIC kwenye Maonesho hayo wameonekana wakivutiwa sana na huduma za Shirika hilo ikiwemo Elimu ya Bima hususani ya Mazao ambayo ni bidhaa mpya iliyotokea kuwa msaada na kimbilio kwa wakulima na wafugaji.
Prosper Peter ni Mratibu wa Bima za mazao na Mifugo kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC) anasema kuwa tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa wadau wa sekta ya Kilimo na Mifugo kujitokeza kujiunga katika Bima hiyo ambapo mpaka sasa kuna zaidi ya wakulima 500 tayari wamejiunga na huduma hiyo.
Kuhusu Mifugo Prosper anasema kuwa, mpaka sasa kuna zaidi ya mifungo 1000 iliyofikiwa na Bima hiyo ambapo katika kuitambua mifugo hiyo kumekuwepo na kifaa maalumu ambayo ni heleni (Ear Tags) anayovalishwa mfugo mmoja hasa kwa Ng’ombe wa nyama na maziwa.
“Kifaa hiki kina usalama sana, mfugo akishavalishwa hakiwezi kutumika kwa mwingine hata kama kitakuwa kimevuliwa, hivyo atatakiwa awe nacho muda wote” anasema Prosper.
Ameitaja mikoa ambayo wafugaji wake wamefikiwa na huduma hii ni pamoja na Mbeya, Tanga na Kilimanjaro, na kwamba NIC inaendelea kuwahamasisha wafugaji katika mikoa mingine kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo ili kujihakikishia usalama wa mifugo yao pale wanapopatwa na majanga mbalimbali na kupelekea kifo.