Mfumo wa kieletroniki wa kuendesha na kuwasiliana na vifaa vya umwagiliaji shambani kwa njia ya simu uliobuniwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Muonekano wa ndege isiyo na rubani maarufu kama Droni ambayo mkulima anaweza kuitumia kukagua shamba lake kwa kupiga picha.
Fundi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Bakari Abdallah Kushoto akiwa na Rabo Humphrey mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu fani ya Uhandisi wa Kilimo wakiwa wameshika ndege isiyo na rubani inayotumiwa na wakulima kukagua mashamba.
Mtaalamu wa udongo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Louis Mdoe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye Banda la SUA lililopo kwenye maonesho ya nanenane kanda ya Mashariki mkoani Morogoro.
NA: FARIDA SAID, MOROGORO.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimekuja na teknolojia mpya ya mfumo wa umwagiliaji kwa kutumia simu ya mkononi ambayo itampa mkulima fursa ya kumwagilia mazao shambani akiwa mahala popote kwa kutumia simu ya mkononi.
Mfumo huo ambao hauchagui aina ya simu, mkulima anaweza kuutumia katika kumwagilia shamba, kunyunyiza viua dudu kwenye mimea na mifugo kwa kuunganisha na mtambo wa maji ambao atakuwa umefungwa kwenye eneo lake.
Akizungumza kwenye maonesho ya wakulima Nanenane kanda ya mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro fundi kutoka Shule Kuu ya Uhandisi Kilimo SUA, Fundi Bakari Abdallah amesema kuwa mfumo huo unamrahisishia mkulima mdogo kuweza kumwagilia shamba lake akiwa mahali popote bila ya kujali umbali.
“Mfumo huu anaweza kuutumia akiwa popote hata ukiwa Mwanza shamba lipo Morogoro unaweza kuupa amri ya kuwasha na kuzima mitambo ya umwagiliaji kwa kutuma ujumbe wa maandishi kupitia simu ya mkononi.” amesama Fundi Abdallah.
Amesema mfumo huo unaweza kuunganishwa na simu ya aina yeyote na mahala popote ambapo kuna mawasiliano ya simu kwani unatuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa kuandika neno washa kama mkulima anataka kumwagilia na neno zima baada ya kumwagilia.
Aidha amesema mbali na mfumo huo pia wana teknolojia ya kukagua shamba kwa kutumia ndege isiyo na rubani maarufu kama Droni ambayo mkulima anaweza kuitumia kukagua shamba lake kwa kupiga picha na kutambua ni sehemu gani ya shamba lake kuna mazao yamekaa vibaya au vizuri kwa urahisi zaidi.
Ndege hiyo pia inaweza kutumika katika kupanga mipango miji kwa kutambua maeneo ambayo yemejengwa na yasiyojengwa pamoja na kutambua mahitaji ya huduma za kijamii.
Kwa upande wake mtaalamu wa udongo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Louis Mdoe amewataka wakulima kuacha tabia ya kupima udongo kwa macho badala yake wapime udongo kupitia wataalamu ili kutambua aina ya udongo na virutubisho vinavyopatikana kwenye udongo pamoja na aina gani ya mbolea anapaswa kutumia.
Amesema kuna faida nyingi kwa mkulima anapopima udongo kwani anaweza kutambua aina gani ya mazao yanaweza kustawi katika shamba lake pia aina gani ya mbolea anapaswa kutumia ili kupata matokea yenye tija wakati wa mavuno.
Katika msimu huu wa Nanenane wakulima wameshauriwa kufika katika banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ili kupata elimu kutoka kwa wataalam wa kilimo pamoja na ushauri wa kilimo bora na kilimo biashara.
Pamoja na elimu pia SUA inatoa huduma mbalimbali kwa wakulima ikiwemo ya upimaji wa udongo ambapo mkulima anatakiwa kufika na sampuli ya udongo kwenye banda la SUA ambapo huduma hiyo inatolewa bila ya malipo katika kipindi hiki cha nanenane.
MWISHO.