NA: NAMNYAK KIVUYO ARUSHA.
kitengo cha wanawake chama cha waalimu Tanzania mkoa wa Arusha wamesherekea wiki ya wanawake kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kwa kuasaidia mahitaji mbalimbali watoto wenye mahitaji maalum katika shule msingi Patandi.
Akiongea na wandishi wa habari wakati wakitoa misaada hiyo mwenyekiti wa kitengo hicho mkoa wa Arusha mwalimu Anna Kaaya alisema kuwa wameona waje washirikiane na watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwapelekea mahitaji mbalimbali kama vile sabuni, taulo za kike, mafuta ya kujipaka, sukari na vitu vingine.
Mwalimu Kaaya alisema katika tukio hilo wamebeba ujumbe muhimu wa kuwakumbusha wanawake wote kuna huduma muhimu wanatakiwa kulitekeleza katika shule hiyo kwa kujitoa kwa moyo kuwasaidia watoto hao lakini pia wanawake wote ambao wametokea kupata watoto wa aina hiyo wasione kama ni mkosi au laana bali ni mpango wa Mungu
Mratibu wa kitengo hicho Mwalimu Magdalena Mhina alisema kuwa wanaamini kuwa watoto hao ni walimu wa baadae wakiwasimamia na kuwajenga zaidi wanaweza kuja kuwa walimu wazuri wa elimu maalum ambapo hawataishia hapo katika kuwasaidia kwani watatengeneza mpango wa kufanya harambee kwaajili ya kuwawezesha kupata bima ya afya.
Mwalimu Jane Twahira mweka hazina wa kitengo hicho alieleza kuwa katika kusherekea siku ya wanawake Duniani wanawatia moyo zaidi walimu wanao wahudumia watoto hao kwasababu kazi hiyo inahitaji moyo wa dhati na upendo wa dhati hivyo waendelee kuwalea kwa upendo na kuwahudumia kwa upendo.
“Watoto hawa kikubwa wanachokihitahi ni upendo yaani anavyopendwa ni rahisi kufundishika na kwasababu chama cha walimu kinahudimia walimu sisi leo tumekuja kuwatia moyo,” alisema.
Mwalimu Betha Gerald mjumbe wa kamati ya taifa ya chama cha walimu anayewakilisha mkoa wa Arusha alisema kuwa wameenda kutembelea walimu wenzao lakini pia kuona kazi wanayoifanya kwa watoto ambapo wameguswa na mahitaji ya watoto kwani sio rahisi kwa mtu ambaye yupo nje kuambiwa na akaelewa lakini wakiona wanaweza kuona changamoto iliyopo.
“Tumewaona watoto na tumeona hali zao, kwakweli wanahitaji kusaidiwa na tumeona wanachangamoto kubwa ya bima za afya, tunawaomba wadau wanaoweza kuchangia watoto hawa wakapata bima tutashukuru sana lakini pia sisi kama chama cha walimu tutaangalia jinsi gani tutaweza kutoa ili kusaidia kazi ya walimu wenzetu kuwa rahisi,” Alieleza.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Patandi Jackline Mtui alisema kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wapo 110 ambapo wapo wenye ulemavu tofauti tofauti wasiona, viziwi, ulemavu wa akili na usonji na msaada huo waliowapatia utawasaidia sana lakini pia wanawakaribisha wadau wengine kuweza kuwasaidia.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni bima kwaajili ya watoto hawa kupata matibabu wanapougua hasa wanaokaa bweni, wakiugua tunakimbizana huku na huku kupata matibabu yao kwahiyo tukipata msaada wa bima itatusaidia sana,”alisema.