Home LOCAL MAVUNDE “ASA HAKIKISHENI MNAONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU BORA KUKIDHI MAHITAJI HALISI YA...

MAVUNDE “ASA HAKIKISHENI MNAONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU BORA KUKIDHI MAHITAJI HALISI YA WAKULIMA”.


waziri wa Kilimo Antony Mavunde akisikiliza jambo kuhusiana na shamba la mbegu la ASA kutoka kwa mkurugenzi mtendaji wa wakala wa mbegu za kilimo nchini Dkt Sophia Kashenge


Naibu waziri wa kilimo Antony Mavunde akiongea na wafanyakazi wa shamba la wakala wa mbegu ASA Arusha baada ya kutembelea mashamba hayo.

Mkurugenzi mtendaji wa wakala wa mbegu za kilimo nchini Dkt Sophia Kashenge akiongea katika eneo la shamba la Tengeru linalomilikiwa na wakala huyo

NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA

Naibu waziri wa kilimo Antony Mavunde ameitaka wakala wa uzalishaji wa mbegu za kilimo nchini (ASA) kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa mbegu bora ili kuweza kukidhi mahitaji halisi ya wakulima kwani kwasasa wanazalisha tani 7000 kwa kushirikiana na taasisi binafsi huku mahitaji yakiwa ni tani laki tatu.

Mavunde aliyasema hayo wakati alipotembelea mashamba ya wakala huyo katika eneo la Ngaramtoni na Tengeru mkoani Arusha ambapo alisema kuwa serikali imeamua kufungua masoko ya nje hivyo ni lazima wafanye kazi ya kuzalisha mbegu kwa wingi ili waweze kuweka malengo ya kuhakikisha sekta hiyo inaongeza mauzo.

“Moja kati ya changamoto ya uuzaji wa nje ni upatikanaji wa mzigo wa kutosha hivyo lazima tuongeze uzalishaji kwa kufanya tafiti mbalimbali kupitia TARI na sisi kama ASA tufanye kazi yetu ya kuzalisha mbegu na kuzipeleka kwa wakulima na hii itatusaidia kuweza kufikia masoko makubwa tuliyoyafungua,”alisema Mavunde.

“Kwenye eneo hili la mboga mboga na matunda kama serikali tumejiwekea malengo ambapo tunataka sekta hii iongeze mauzo kutoka milioni 750 za Dola za Marekani kwenda hadi bilioni 2 kwanzia 2030 ambapo mchango wa sekta hii ni mauzo ya zaidi ya dola milioni 700 lakini tunataka ikue ili tuwe na mauzo ya Dola bilioni mbili kila mwaka,”Alieleza.

Alieleza kuwa malengo hayo hayawezi kufikiwa pasipo kuzalisha mbegu bora na miche bora kwa wingi na kwa uhakika zaidi ambapo wizara itaendelea kuiwezesha  ASA, TARI na TOSCI kufikia malengo hayo kwani wanataka Tanzania itambulike Dunia nzima kupitia mboga mboga na matunda ikiwa jambo hilo linawezekana.

“Mwenyezi Mungu amewajalia wana ardhi yenye rutuba ambayo wakiitumia vizuri inaweza kuleta manufaa makubwa kwenye ujenzi wa uchumi wa Taifa letu lakini pia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kuongeza ajira na kupunguza umasikini lakini pia tumeona kuna mambo ambayo tunahitaji kuyawekea mkazo zaidi mojawapo ikiwa ni kuendelea kuwaelimisha wakulima walime katika kanuni bora za kilimo na kuwaletea tija,”alisema.

Alifafanua kuwa tayari wameshapata masoko ya uhakika ya parachichi ambapo wanapeleka India, Afrika kusini na Kenya lakini pia wapo katika majadiliano ya mwisho na China na Marekani ili kufungua masoko ya mboga mboga na matunda katika nchi hizo

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa wakala wa mbegu za kilimo nchini Dkt Sophia Kashenge alisema kuwa kwasasa wameongeza uzalishaji tofauti na awali kwasababu ya msukumo wa serikali na uwezeshwaji umekuwa wa tofauti na awali kwani mashamba hayo yalikuwa hayatunzwi kutokana na ukosefu wa fedha ila baada ya serikali kujua umuhimu wa mbegu  sasa hivi imekuwa ni kipaumbele cha wizara ya kilimo.

Alisema kwa miaka minne iliyopita walikuwa wanazalisha tani 520 lakini kwasasa hivi wameongeza uzalishaji na kufikia tani 3033 ambapo malengo yao kwa msimu unaokuja wanategemea kuzalisha tani 6000 ambapo watatumia maeneo hayo vizuri kwani wanashindwa kufikia malengo kwasababu wanatumia mvua zaidi.

“Kulikuwa na mabadiliko ya hali hewa, tukajikuta mvua zinabadilika hali iliyopelekea uzalishaji kupungua kama mnavyoona vitunguu mahali hapa vimekuwa hivyo kwasababu hatukutegemea kama mwezi wa pili kutakuwa na mvua ambazo zilizidi na tukapata uvamizi wa fangasi na madhara mengine,” alisema Dkt. Kashenge.

Alisema kwasasa wanaenda vizuri na wanaamini watafikiwa lengo ambapo  shamba la Arusha lina hekta 600 na eneo linalofaa kulimwa likitolewa maeneo ya makorongo na maeneo yaliyojengwa inabaki hekta 500 na msimu uliopita wamefanikiwa kulima hekta 440 na kupata takribani tani 600 na msimu huu wamelilima lote.

Alifafanua kuwa katika uzalishaji wa mbegu wanahitaji maeneo makubwa kwasababu ni lazima kila mbegu iwe na eneo la utengano baina ya mbegu na mbegu ili kuzuia uchavushaji ambapo ni kutenganisha baina ya mbegu na mbegu kwa kilometa 1.5 hadi 3.

Previous articleTGNP YASHIRIKI KONGAMANO LA KITAIFA LA WANAWAKE JIJINI ARUSHA
Next articleBOHARI YA DAWA (MSD) IMETUMIA BILIONI 16.7 UJENZI KIWANDA CHA MIPIRA YA MIKONO (GLAVES) NA DAWA IDOFI MAKAMBAKO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here