Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kusajili miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 8,129.3 ambazo ni sawa na Shilingi trillion 18.75 inayotoa ajira takribani 62,301 kuanzia Machi, 2021 hadi Februari, 2022 ikilinganishwa na 2020/2021 ambao ulikuwa ni dola za kimarekani billion 1 tu.
Akiongea Machi 10, 2022 Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha mwaka mmoja madarakani, Dkt Kijaji amesema hati za makubaliano 37 zenye thamani ya dola za marekani bilioni 8, ambazo ni sawa na Shilingi 18.5 trilioni zinazotarajiwa kuzalisha ajira takriban 214,575 zilisainiwa wakati wa Maonesho ya Expo 2020 Dubai.
Aidha Dkt Kijaji alitaja Mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishaji wa Kongano za Viwanda kwa lengo la kuwasaidia wakulima wadogo na wawekezaji wa ndani. Kongamano hizo ni pamoja na ujenzi wa Kongano ya Viwanda vya Mafuta ya Kula mkoani Singida yenye ukubwa wa ekari 45,000, Kongano la Sukari (Sugar Park) katika eneo la Dakawa na Kongano ya Viwanda Kwala Pwani yenye ukubwa wa ekari 2,500.
Mafanikio makubwa mengine ni Ujenzi Kongano za Viwanda vya Elsewedy Kigamboni lenye ukubwa wa Mita za Mraba milioni 2.2 ambapo uwekezaji wake unakadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 400. Takriban viwanda 100 na ajira za moja kwa moja 50,000 zitazalishwa katika kongani hii ya viwanda Kigamboni. Alisema Dkt. Kijaji.
Ili Kukabiliana na uhaba wa mbolea na kupitia makongamano ya Biashara na Uwekezaji Serikali imewezesha kupatikana kwa mwekezaji wa Kiwanda cha Mbolea kinachoitwa ITRACOM Fertilizer Tanzania Limited kitakachowekeza mtaji wa kiwanda hicho Dola za Kimarekani milioni 180 na kitaajiri wafanyakazi wa kudumu takriban 3000 na kitakuwa na uwezo uliosimikwa wa kuzalisha mbolea tani 500,000 kwa mwaka.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuunganisha na kufungamanisha mifumo ya kielektroniki ya utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni na Upatikanaji wa Ardhi ya Uwekezaji pamoja na kutengeneza mfumo wa pamoja wa kurahisisha uwekezaji (Tanzania electronic Investment Window (TeIW) unalenga kuunganisha kwa njia ya kielekroniki huduma zote zinazotolewa na taasisi 12 za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mahali pamoja (One Stop Shop). QMESEMA Dkt. Kijaji.
Serikali imefanikiwa kuvitafutia ufumbuzi vikwazo 42 kati ya vikwazo 64 vilivyokuwa vinawakabili wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya. Pia imefanikiwa kuridhia Mkataba wa kujiunga na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) utakao toa soko kubwa barani Afrika lenye takriban watu bilioni 1.3 na pato ghafi la jumla ya kiasi cha trilioni 3.4. kupitia mkataba huu Tanzania itanufaika kwa kuuza bidhaa na huduma. ALISEMA Dkt. Kijaji
Aidha,amesema Serikali imefanikiwa kuchukua hatua za makusudi katika kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo (Machinga), kwa kutatua tatizo la maeneo ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo (Machinga) kwa kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa kwa kushirikiana na machinga kutenga maeneo wezeshi na yanayofikika na wateja ili kuongeza tija, mapato na kuongeza ajira.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu pia imewezesha uhumizaji wa Mafunzo kwa Wajasiriamali ambapo kupitia maelekezo yake jumla ya Wajasiriamali 4,156 (wanaume 1,662 wanawake 2,494) wamepatiwa ujuzi na mafunzo katika nyanja za Ujasiriamali, Usimamizi wa Biashara na Usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na madini.
Aidha, amesema Serikali ya awamu ya sita imewezesha upatikanaji wa majengo mapya matano (5) ya viwanda yenye thamani ya shilingi bilioni moja yamejegwa katika mikoa ya Katavi (2), Mwanza (1) na Morogoro (2). Majengo hayo yanatarajiwa kuwezesha viwanda vidogo 10 kuanzishwa katika mikoa hiyo.
MWISHO