Na.Faustine Gimu ,Elimu ya Afya,Idara ya Kinga,Wizara ya Afya[MOH-
Katika kusherehekea Sikukuu za Mwaka mpya 2023,baadhi ya Wananchi katika mikoa ya Dodoma na Mtwara wamevutiwa na hatua ya serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini .
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi hao akiwemo Meshack Michael Mkazi wa Ntyuka mkoani Dodoma kwa upande wake amesema mwaka 2022 serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya huku matarajio yake mwaka 2023 ni kuona kasi ya utoaji wa huduma bora za afya mwaka 2023.
Naye Mzee Keneth Mshama mkazi wa Masasi mkoani Mtwara ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa kuweka kipaumbele cha kutoa taarifa na elimu mapema mara tu panapotokea mlipuko wa magonjwa katika kuchukua tahadhari.
Ikumbukwe kuwa serikali ya awamu ya sita imewezesha ujenzi wa zahanati 786,vituo vya afya 471,ujenzi wa hospitali za halmashauri 154 zimeendelezwa pamoja na kukarabatiwa.
Aidha,kwa mara ya kwanza Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amewezesha ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za dharura 80,majengo ya kutolea huduma za wagonjwa mahututi[ICU]28, mitambo ya kuzalisha hewa ya Oksijeni 21,kusambaza mashine za X-ray 137 kwenye vituo vya kutolea huduma ,kuajiri watumishi kada ya afya 7736,na ujenzi wa nyumba za watumishi 150 two in One.
Pia,Serikali kupitia wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa taarifa na kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya afya ambapo Kongamano la kwanza la Maendeleo ya Habari lilifanyika jijini Dar Es Salaam na mgeni Rais ,Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ,Mhe.Nape Nnauye huku katika kongamano hilo likizitunuku wizara 10 zilizofanya vizuri katika utoaji wa habari nchini katika kipindi cha mwaka 2022 na Wizara ya Afya ikiibuka kidedea.
Hii ni tuzo ya pili kwa Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini baada ya mwezi Februari 2022 kupata tuzo ya mshindi wa kwanza upande wa Wizara kutoka Tanzania Digital Award iliyotambua mchango wa Wizara kuhabarisha umma kupitia mitandao ya kijamii.
MWISHO.