Na: WAF- DSM.
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuja na mkakati wa kushirikisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika ajenda ya ubora wa huduma kwa wananchi ikiwa ni ajenda ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyoanza kutekelezwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.
Dkt. Mollel amebainisha hilo leo Januari 3, 2023 katika kikao kazi na Watumishi wa hospitali za Mnazi mmoja, Kigogo na Hospitali ya Wilaya ya Ubungo baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya upatikanaji na ubora wa huduma katika hospitali hizo.
“Sisi Wizara ya Afya na TAMISEMI tumekuwa tukiwajengea uwezo Watumishi na viongozi wa huduma za afya kusaidia kutoa huduma bora kwa Wananchi lakini tukasahau kuwajengea uwezo wenye nyumba ambao ni Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili wajue huduma bora na waweze kusimamia vizuri huduma hizo katika maeneo yao.” Amesema.
Ameendelea kusema kuwa, tayari Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR TAMISEMI imekubaliana kwa pamoja kuendelea kushirikiana na viongozi wote katika ngazi ya Mkoa ili kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi wa hali zote za kiuchumi.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema, tayari Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameweka mikakati mizuri ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa inakuwa ya kutosha katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
Aidha, Dkt. Mollel ameelekeza Wataalamu katika vituo vya kutolea huduma za afya kuendelea kufuata miongozo na Sera ya Wizara ya Afya katika kutoa huduma kwa wananchi hasa kwa makundi maalumu kama vile wazee, watoto na wajawazito.
Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema Serikali inaendelea kuboresha utaratibu wa Rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine ili kuhakikisha usalama wa afya ya mgonjwa na kuepusha vifo vinavyoweza kuzuilika.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amebainisha, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI inatarajia kuwa na kikao cha pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa, Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Wilaya ili kuweka utaratibu mzuri wa Rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kingine na kuondoa changamoto zinazoweza kuzuilika.
Mbali na hayo Dkt. Mollel amemshukuru Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Viongozi wa chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia vizuri utoaji huduma katika maeneo hayo, hali iliyosaidia kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi yanayoweza kuzuilika.
Mwisho.