NA: NAMNYAK KIVUYO,ARUSHA.
Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Meru imemuagiza mhandisi wa wilaya hiyo Arstedius Msuta kumsimamisha kuendelea na ujenzi fundi anayejenga nyumba za watumishi katika shule ya sekondari elimu maalum iliyopo eneo la Patandi na kumpa kazi hiyo fundi mwingine kutokana na ujenzi kusuasua.
Akiongea katika ziara yao kukakugua miradi mbalimbali mwakilishi wa mwenyekiti wa kamati ya siasa Gurisha Mfanga alisema kuwa fundi huyo ameshindwa kukamilisha kazi aliyopewa kwa wakati ambayo ni kujenga nyumba za watumishi za mbili ndani ya moja kwa muda uliotakiwa ambapo alitakiwa kukamilisha ujenzi huo Januari 2022.
“Alitakiwa kukamilisha Januari sasa ni machi na ndio kwanza anaanza msingi wa nyumba ya pili na hii ya kwanza bado haijakamilika hata tukisema abaki hadi kufika Aprili 15 ambayo ndio mwisho wa muda wa nyongeza hawezi akawa amekamilisha kwahiyo Injinia waambie hawa mafundi waliopo hapa waache kwanzia sasa tafuteni fundi mwingine yeye amalizie hii ambayo ipo katika hatua za mwisho,” Alisema Gurisha.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alisema kuwa kwa maslahi mapana ya nchi ni vema akapewa fundi mwingine kazi ya kujenga nyumba ya pili kwani fundi huyo ameonyesha kushindwa kuliko pitiliiza lakini pia itakuwa ni fundisho kwa mafundi wengine ambao wanaomba kazi ila kuzifanya inakuwa mtihani.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru Mwalimu Zainabu Makwinya alieleza kuwa ni kweli mradi huo umechelewa lakini walishakaa kikao na kuagiza fundi huyo aondolewe na mwingine aanze kazi ambapo fundi mpya ameshapatikana na atakabidhiwa kazi hiyo.
Naye mkuu wa shule ya sekondari Patandi elimu maalum mwalimu Janeth Mollel akielezea taarifa ya ujenzi huo alis ma kuwa fundi huyo alijaza mkataba wa kujenga majengo hayo Novemba 26, 2021 na kutakiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 26,2022 ambapo alitakiwa kuanza nyumba hizo kwanzia msingi hadi kukamilika.
“Hadi sasa nyumba ya kwanza ipo katika hatua ya uwekaji mfumo wa maji safi na maji taka na ya pili ipo katika hatua ya kujengea msingi na kumwaga jamvi na nyumba zote hizi mbili ni two in one ambapo nyumba ya kwanza mpaka Sasa imegharimu zaidi milioni 48 na salio lililopo ni zaidi ya milioni 50,”alisema Mwalimu Mollel.
Aidha kamati hiyo pia ilitembelea miradi mingine ikiwemo shule mpya ya sekondari Ambureni ambayo ina miradi yenye thamani ya shilingi milioni 470 ambapo waliwataka viongozi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wanafunzi wanaendelea kunufaika kwa kupata elimu bora katika umbali mdogo.
Katika mradi huo mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl.Zainabu Makwinya aliishukuru serikali kwa kutoa fedha za maendeleo ambapo imetoa shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika shule hiyo mpya lakini pia imetoa milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya Madarasa vilivyokamilika.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe.Mhandisi Richard Ruyango alisema wilaya hiyo inaendelea Kutekeleza Ilani ya CCM kwa kuhakikisha miradi inatekelezeka kama ilivyokusudiwa ambapo ameelekeza Halmashauri kuhakikisha mafundi wanafanya Kazi kwa muda uliokusudiwa.
Hata hivyo ziara hiyo ya kamati ya siasa kwa siku ya kwanza imeweza kufikia miradi inayoendelea kwenye Shule mpya ya Ambureni ,mradi wa maabara za biolojia na chemistry sekondari Patandi maalum na ujenzi wa nyumba mbili za waumishi, ujenzi wa jengo Maalum katika Hospitali ya wilaya hiyo pamoja chumba cha darasa katika shule ya sekondari Siela.