Askofu Mkuu wa Kanisa la ABC Tanzania lililopo Mtaa wa
Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila (kushoto)) akizungumza na wajane na wagane wakati wa hafla ya kukabidhi msaada
wa chakula (mchele) nguo na fedha iliyofanyika leo Desemba 26, 2022.
Picha ya pamoja baada ya kutolewa kwa msaada huo.
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam.
KANISA la Abundant Blessing Church (ABC) lililopo Mtaa wa Mandela jijini
Dar es Salaam limetoa msaada wa chakula, nguo za aina mbalimbali, viatu na fedha kwa
ajili ya kuwasaidia Wagane na Wajane 40 wanaoishi kwenye mtaa huo..
Akizungumza wakati wa kukabidhi
msaada huo Askofu mkuu wa kanisa hilo hapa nchini, Flaston Ndabila alisema wamekuwa wakiguswa na
changamoto mbalimbali za Wajane na wagane na makundi mengine yanayoishi jirani
na kanisa hilo na maeneo mengine ya jirani na kuwa wameweka utaratibu kila mwaka kutoa msaada
huo.
“Huu ni mwaka wetu wa sita tumekuwa tukifanya hivi hasa kipindi hiki cha Sikukuu za mwishoni mwa
mwaka za Krismas na mwaka mpya na leo tumetoa msaada huu ikiwa ni kuadhimisha
siku ya kupeana zawadi baada ya krismas (Boxing day) alisema Ndabila.
Ndabila alisema kutoa msaada kwa makundi hayo ni kuchota baraka kutoka kwa
Mungu kwani hata vitabu vya dini zote ya kikristo na kiislam vinaeleza hivyo.
Ndabila alisema nguo hizo zimetolewa na waumini wa kanisa hilo kwa ajili ya
kusherehekea boxing day kwa makundi hayo.
Baadhi ya wagane na wajane waliopata
msaada huo waliushukuru uongozi wa kanisa hilo kwa msaada ambao wamekuwa
wakiutoa kwako hasa Askofu wa kanisa hilo, Flaston Ndabila na mke wake Janeth
Ndabila.
“Kwa kweli hatuna cha kueleza zaidi ya kutoa shukurani zetu na Mungu
awape afya njema na maisha marefu” alisema. Khadija Hamisi.
Mjumbe wa Serikali ya mtaa huo, Juma Hassan alisema kanisa hilo limekuwa la
mfano katika kusaidia jamii ya eneo hilo kwa mambo mbalimbali na hata wakati wa
mafuriko limekuwa likijitoa kurekebisha miundombinu pamoja na kuwafariji
wahanga.
“Kanisa la ABC hakika ni kanisa lenye uongozi thabiti limekuwa
likishirikiana na Serikali kwa mambo mengi na hata kuwanunulia madaftari na
vifaa wanafunzi ambao hawana uwezo” alisema Hassan.
Alisema Askofu wa kanisa hilo Flaston Ndabila kila inapofika mwishoni mwa
mwaka amekuwa akiwakumbusha kwa ajili ya kutoa misaada hiyo japo ambalo
linapendeza hata mbele za Mungu.