WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya maboresho makubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Amesema kuwa katika kutimiza hilo hivi karibuni imetoa fedha kwa ajili kununua vifaa vya kisasa ikiwemo MRI ambayo inaweza kumpima mgonjwa hata akiwa na chuma mwilini.
“Sambamba na huduma hizi nzuri zinazotolewa na wataalam wetu kwa moyo mkubwa Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika hospitali yetu ya Taifa ili iendelee kutoa huduma bora na za kisasa zaidi.”
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Desemba 23, 2022) baada ya kufanya ziara katika hospitali hiyo na kuzungumza na wagonjwa na wauguzi ambao wamemueleza kuwa huduma zinazotolewa hospitali hapo zinaridhisha.
Pia, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na huduma za matibabu zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na amewapongeza watendaji wa hospitali hiyo kwa kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Akizungumzia suala la gharama kubwa za matibabu ambalo limelalamikiwa na wananchi wengi wanaouguza ndugu zao, Waziri Mkuu amesema mpango wa bima ya afya kwa wote unakwenda kumaliza changamoto hiyo.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Watanzania ambao wanashindwa kumudu baadhi ya huduma za matibabu wawasilishe masuala yao katika ofisi ya Ustawi wa Jamii zilizopo kwenye hosptali husika na watapewa maelekezo ya kufuata ili wapate msamaha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohammed Janabi amewasisitiza wagonjwa wote ambao hawana uwezo wa kulipia huduma hizo mbalimbali zitolewazo hospitalini hapo wafuate taratibu watahudumiwa. “Kila mwezi hospitali inatoa msamaha wa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa wasiokuwa na uwezo.”
Wakizungumzia kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wanaouguza ndugu zao katika hospitali hiyo wamesema kuwa huduma zitolewazo ni nzuri na hakuna anayeombwa rushwa ila changamoto waliyonayo ni kwamba matibabu yanatolewa kwa gharama kubwa.