LAILAH Ngozi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amewataka Watanzania kuendelea kumwamini Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa, nchi ipo kwenye mikono salama.
Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Rais Samia kuelezwa kushangwazwa na taarifa zilizotolewa kwamba, nchi haina fedha na kwamba imekopa sana.
Akizungumza katika utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Reli ya SGR kuanzia Tabora mpaka Kigoma tarehe 20 Desemba 2022, Rais Samia alisema wanaotoa pata hamu ya kutoa taarifa ndani ya Wizara ya Fedha kuhusu matumizi ya fedha, watoe ufafanuzi zimekwenda kufanya nini.
“Mwezi huu kumekuja vijimaneno maneno kwamba, pesa hakuna serikalini, ndio hakuna kwa sababu kwanza mikopo tuliyokopa imechelewa…, kwa kuweka heshima ya nchi yetu lazima tulipe. Matumizi ya ndani tutajibana, tutajifunga mkanda mengine yaende.
“Niwaambie Wizara ya Fedha, taarifa hizi zinatoka huko kwenu. Kwa hiyo angalieni humo ndani, wanapopata hamu ya kutoa taarifa, basi watoe na hayo maelezo kwamba kuna hiki ndio.. lakini maelezo yake ni haya,” alisema Rais Samia.
Akizungumzia taarifa hiyo, Ngozi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitoa taarifa zisizo sahihi kwa lengo la kuchonganisha Serikali ya Rais Samia na wananchi wake, akisisitiza jambo hilo halina afya kwa taifa.
“Miradi ambayo rais anawekeza, itasaidi itasaidia wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, wito wangu tumpe ushirikiano rais ili amalize miradi kwa wakati. Mpaka sasa hakuna hata mradi mmoja uliosimama.
“Ndugu zangu, kuna watu hawaitakii mema nchi yetu…, niwatoe hofu kwamba, Rais Samia ana nia thabiti kwa wananchi wake, haya yote ni kwa faida ya nchi yetu,” amesema.
Mjumbe huyo amesema, ni vema kwa wanachama wa chama hicho kujenga utamaduni wa kutoa ufafanuzi kwa wananchi pale taarifa za upotoshaji kuhusu Rais Samia na serikali yake zinapozusha katika jamii.
Amesema, Ilani ya chama hicho ya 2020 – 2025 ilijielekeza kujikita katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ili kuboresha jamii, kiuchumi na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo.
“Serikali itaendelea kukopa kwanye baadhi ya miradi ambayo baada ya kukamilika kwake, itakuwa vyanzo vipya vya mapato. Niwatoe hofu, miradi hii itajilipa yenyewe,”amesema.
Rais Samia katika sherehe ya kutia Saini ya ujenzi wa reli hiyo, alisisitiza kwamba nchi inakopa kwa ajili ya faida ya sasa nay a baadaye.
“Tunakopa ili tujenge leo kwa maendeleo ya leo na baadaye, kila pale tunapohisi kuna faida tutaendelea kukopa. Na waseme sana, waseme pia ndio awamu iliyojenga sana,” alisema.