NA MWANDISHI WETU
MSANII wa muziki wa Kizazi Kipya Abdul-Azizi Haji ‘Wyse Tz,’ anayetamba na ngoma ya Butterfly aelezea kuwa wimbo huo umempa mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi.
Nyota huyo ambaye aliwahi kutamba na ngoma ya Bado kidogo ambayo alifanya na Ben Pool, Harusi alio mshirikisha Jovial kutoka Kenya pamoja na ngoma ya Mama.
Akizungumza na Ukurasa huu amesema ngoma ya Butterfly, imefungua milango kwa kiasi kikubwa katika safari yake ya muziki na kumfanya kupata michongo mingi.
“Nina furaha kubwa kwa kuwa muziki wangu umeanza kunipa mafanikio makubwa ambayo yanaenda kutimiza ndoto zangu katika tasnia hii ndani na nje ya nchi yetu,”anasema Wyse Tz.
Aliongeza kuwa kwa sasa amekuwa akipata shoo nyingi nje ya nchi ikiwemo Kenya jambo ambalo limekuwa mbaraka kwake kwa kuongezeka kipato.
Aidha alisema kwa sasa hajafikiria kufanya kolabo na msanii nje ya Afrika bado anataka kufanya na wasanii wanaofanya vizuri ulimwenguni kutokea bara hili.
“Nina mpango wa kufanya kolabo na Mr.Eazi ambaye tunazungumza mara Kazaa lakini pia Joe Boy ambaye tulikua nae wote kwenye project ya EMPAWA 100 iliyo chini ya Mr.Eazi.”
Pia alisema yupo mbioni kutoa EP yake ambayo itakuwa na ngoma nne ambazo anafikiria kushirikisha na wasanii wengine kutoka sehemu tofauti katika ukanda wa Afrika.