Mvutano wa kibiashara wa makampuni ya Nanovas na Extrabet kuhusu Betpawa, bado utata
Wakati kuna madai ya kubadilishwa kinyemela ushirikiano wa kibiashara wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Betpawa ya Seychelles, ambayo inafanya kazi na kampuni yake mama iliyopo Uingereza ya softpawa, kutoka kampuni ya Nanovas (T) Ltd kwenda kampuni ya Extrabet . Tume ya taifa ya ushindani wa kibiashara nchini (FCC) imesema haina taarifa ya mgogoro wa kibiashara baina ya makampuni hayo yanayojishughulisha na michezo ya kubahatisha.
Awali kampuni ya Nanovas ilikuwa ikishirikiana kibiashara na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Betpawa kutoka Seychelles ambayo inafanya kazi na kampuni yake mama ya Softpawa ya nchini Uingereza na hivi karibuni ilipotangaza kusimamisha huduma kwa ajili ya kuboresha miundombinu yake, Betpawa ikaanza kufanya kazi na kampuni ya Extrabet iliyosajiliwa kwa haraka katika kipindi hicho hatua iliyozua sintofahamu kwa kampuni ya Nanovas kuhusu ushirikiano huo mpya.
Hata hivyo akizungumzia suala hilo jana, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema baada ya kufuatilia kwenye idara za FCC hakuna kesi ya mgogoro baina ya makampuni hayo.
“Mgogoro uliopo unaofanana na huo ni ule kati ya Chama cha makampuni ya michezo ya kubahatisha Tanzania (TSBA) na kampuni ya Vodacom, hatuna kesi ya makampuni hayo uliyoyataja,” alisema Erio.
uchunguzi wetu unaonyesha kuwa waendeshaji wa awali wa chapa ya Betpawa waliachana kibiashara kutokana na madai ya kodi ambayo yalisababisha kampuni ya kigeni ya Softpawa kutolipa deni kubwa la VAT ambalo ni zaidi ya shilingi bilioni 5 za Tanzania ukiachana na penalti za kikodi chini ya sheria na kanuni za mahesabu ya TRA.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo Afisa wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kutoka kitengo cha elimu kwa walipa kodi alisema suala hilo limepelekwa kwenye idara husika na linaendelea kufanyiwa kazi.
“Siwezi kukujibu ‘direct’ swali hilo kwa sababu mpaka nijiridhishe, naweza kukupa email (anuani ya barua pepe) ambapo swali hilo watalijibu kwa ufasaha zaidi,” alisema Afisa huyo.
Inaelezwa sakata hilo la kodi lipo kwenye ofisi ya Kamishna wa Mapato ya Ndani likiendelea kufanyiwa kazi japo kwa kusuasua.
Msemaji wa Bodi ya Michezo ya kubahatisha hakupatikana kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi suala hili jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Michezo ya kubahatisha ni moja ya sekta inayokua kwa kasi nchini na kuchangamsha uchumi huku kampuni tano kubwa zilizowekeza katika sekta hii, zikichangia pato la Serikali kuzidi sekta zingine maarufu kama sekta ya kilimo, Sanaa na hata madini.
Mchango wa sekta ya michezo ya kubahatisha unafikia zaidi ya shilingi bilioni 10 kila mwezi kama mapato ya kodi ya serikali.
Kasi ya ukuaji ambayo sekta ya michezo ya kubahatisha inafikia kila mwaka inaweza kuwa ya kushangaza . Takwimu zinabainisha kuwa katika kipindi chote cha 2015-2021 umekuwa ya kushangaza kwa ukuaji wake, sekta hii imeweza kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi kwa zaidi ya tarakimu mbili kwa mwaka licha ya changamoto mbali mbali kama janga la UVIKO -19.