Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Mary Masanja(Mb) amesema Serikali itaunda Kamati ya kuangalia migogoro ya mipaka na vijiji vinavyozunguka Msitu wa Hifadhi wa Bonde la Wembere uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi kuhusu mgogoro wa mipaka kwenye eneo la ardhioevu katika Kijiji cha Msai na Ujungu mkoani Singida.
Amesema Kamati hiyo itaishauri Serikali endapo kuna umuhimu wa kurekebisha mipaka na kama eneo hilo litafaa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu au la.
“Kuanzia leo tunaunda Kamati ambayo itajumuisha wataalam kutoka ngazi ya Wizara,Mkoa na Wilaya na zoezi hilo litaanza mara moja na itapitia mipaka kwa kushirikiana na wananchi ili kuainisha mipaka halisi kwa kuzingatia ramani iliyopo ili kumaliza mgogoro huo” Mhe. Masanja amesisitiza.
Mhe. Mary Masanja amewataka wananchi hao kuzingatia sheria za kutovamia maeneo ya hifadhi na kuwa walinzi wa eneo hilo mara tathmini itakapokamilika.
Kuhusu changamoto ya wafugaji wanaopitisha ng’ombe katikati ya hifadhi kwa ajili ya kupeleka mifugo yao kunywa maji amesema, Serikali itaangalia namna iliyo bora ya kutatua changamoto hiyo ili wananchi wasiingiliane na masuala ya uhifadhi.
Sambamba na hilo amewataka wananchi waache tabia ya kukata miti hovyo na kukubaliana na mradi wa upandaji miti ulioletwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Naye, Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wa Kata na vijiji kushirikiana na Kamati iliyoundwa wakati wa kupitia upya usahihi wa bikoni zilizowekwa.