WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu washushe mara moja bei walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko na wasitumie kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kupandisha bei.
“Nawasihi wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji. Wale watakaobainika kupandisha bei bidhaa muhimu bila utaratibu hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 6, 2022) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.
Amesema hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko kwenye bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo. “Kufuatia tarifa hizo, niliielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuunda jopo la wataalamu ili kufuatilia taarifa hizo.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Tume ya Ushindani ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini na zile zinazotumia malighafi kutoka nje ya nchi.
“Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na upandaji huo wa bidhaa muhimu. Hatua hizo ni pamoja na usimamiaji wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ambayo inazuia kupanga bei. Hatua nyingine ni Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada.”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wote kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi mahiri na thabiti wa Rais Mheshimiwa Samia kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa.
Amesema ni dhahiri kwamba, matokeo ya utendaji huu yatapunguza umaskini kwa Watanzania na kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuliomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 148.89, ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 101.36 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 47.52 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 132.72 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 127,32 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.4 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa Mwaka 2022/2023, bungeni jijini Dodoma, Aprili 6, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)