Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Bw. Nahmat Mahfoudh akizungumza na Mabalozi Tanzania waliotembelea eneo la ujenzi wa bandari ya Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja. |
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud akizungumza na Mabalozi Tanzania waliotembelea eneo la ujenzi wa bandari ya Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja |
Mabalozi wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Mabalozi unaofanyika mjini Zanzibar wametembelea bandari ya Malindi leo tarehe 17 Novemba 2022 na kujionea jinsi bandari hiyo inavyofanya kazi.
Mabalozi hao pia wametembelea eneo la Mangapwani ambako Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepanga kujenga bandari kubwa mpya na ya kisasa ambayo itaipunguzia mzigo bandari ya Malindi.
Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab imewawezesha Mabalozi hao kujionea jinsi bandari ya Malindi inavyofanya kazi na hivyo kusaidia juhudi za kukuza uchumi wa Zanzibar
Akizungumza na mabalozi hao katika bandari ya Malindi na eneo la Mangapwani, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Bw. Nahmat Mahfoudh amesema bandari ya Malindi kwa sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kupokea makontena mengi na makubwa na meli za kisasa kuliko uwezo wa bandari hiyo ambao ujenzi wake hauruhusu kupokea meli na contena hizo.
‘‘Bandari hii inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa nafasi na uwezo wa kuhudumia meli na makontena makubwa, kwa hiyo bandari hii itabakia kuwa bandari ya meli za abiria kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, kiufupi hii itakuwa bandari ya kitalii’’, alisema Bw. Mahfoudh.
Amesema wameamua kujenga bandari ya mangapwani ili iweze kwenda na mahitaji ya nyakati hizi kwa kuwa uwezo wake ni kupokea Tus 80,000 lakini bandari mpya itakayojengwa Mangapwani itakuwa na uwezo wa kupokea Tus 800,000 hadi 1,800,000.Â
Akiongelea changamoto zinazolikabili Shirika la Bandari Zanzibar Bw. Mahfoudh amesema bado wanapambana kuondokana na madhara yaliyotokana na janga la Covid 19 ambalo limelilitea shirika madhara makubwa.
Akizingumza katika ziara hiyo, Amidi wa Mabalozi nchini, Mhe.Dkt. Asha-Rose Migiro amelishukuru Shirika la Bandari kwa kuwapokea na kuzungumza nao na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya.Â
Amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa utayari wake wa kuwa na Miradi ya kimkakati kama huo wa bandari ya Mangapwani uliopangwa kufanyika katika mkoa wa KaskaziniÂ
Amesema kwa niaba ya mabalozi wenzake wanaahidi kuwa Mabalozi wazuri ambao wataendelea na kazi ya kuwavutia na kuwashawishi wawekezaji wenye mitaji mikubwa ili kuweza kutimiza nia na dhamira ya kuiendeleza Zanzibar.