Home LOCAL SHEREHE YA KUSIMIKA HATMA YA BABA HALISI NA MAMA HALISI KUFANYIKA KESHO

SHEREHE YA KUSIMIKA HATMA YA BABA HALISI NA MAMA HALISI KUFANYIKA KESHO

Baba Halisi na Mama Halisi

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Kanisa Halisi la Mungu Baba kesho Jumapili, litafanya sherehe kubwa ya Kusimika Hatma ya Baba Halisi na Mama Halisi itakayofanyika katika Ukumbi wa Kanisa hilo, lililopo Tegeta Namanga, Kiwanja namba 195, Jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya mwaliko rasmi uliotolewa na Kanisa hilo kwa watu wote wakiwemo Masheikh, Maimamu, Mapadre, Wachungaji, Madaktari na Maprofesa imesema Sherehe hiyo itaanza saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana  na itakuwa ya kihistoria.

“Sherehe hiyo itafanyika lango/tarehe 12 Adari,1(Aprili 10, 2022). Karibu bila kukosa. Ukipata hii habari njema tafadhali mjulishe na mwenzako, kwa maelekezo zaidi wasiliana nasi: 0759 658692, 0629158835”, imesisitiza taarifa hiyo.

Kujua undani wa Sherehe hiyo ya Kusimika Hatma ya Baba Halisi na Mama Halisi, Tafadhali Soma Hapo.

 👇

TOLEO LA PILI
12ADARI,1(MAJIRA HALISI)
1O APRILI, 2022

YALIYOSABABISHA HATMA YA BABA HALISI NA MAMA HALISI ITOKEZE

Kulikuwepo maswali yatokanayo na mistari kadhaa katika kitabu, ambayo yalikuwa bado hayajajibiwa:
KUUFIKIA MLIMA WA NYUMBA YA CHANZO HALISI (Isaya 2:2-4)

Katika mistari hiyo, jambo kubwa ni mlima wa nyumba ya CHANZO HALISI (BWANA) ambao ni imara juu ya milima na vilima!Kitabu kikisema mlima ina maana ya Ufahamu!Hivyo, kinachozungumzwa hapa ni uwepo wa ufahamu mkubwa zaidi unaotoka moja kwa moja kwa CHANZO HALISI ambao uko juu ya ufahamu ule tuliopokea kutoka Mashariki ya Kati kupitia Ulaya, Amerika, Asia, Australia, New Zealand na kadhalika.

Tatizo lililokuwa linakabili ufahamu huo kutoka mashariki ya kati ambao uliletwa Afrika na mataifa ya Ulaya, Amerika na Asia na wakati mwingine Australia na New Zealand ni mistari miwili ya Danieli 7:21 na Ufunuo 13:5-7,ambayo inasema kuwa kila aliyeambatana na ufahamu huo, alishindwa na kujikuta ameishia njiani. Kwa mantiki hiyo, haikuwahi kudhaniwa itakuwa wapi na kwa jinsi gani kuupata huo Mlima wa CHANZO HALISI (BWANA) ambao ni imara juu ya milima na vilima.

KITUO CHA SAUTI
Miaka minne (4) iliyopita, Baba Halisi alifikisha Kanisa kwenye kituo cha Sauti, ambacho kiko juu ya Neno!Hapo ndipo Uzao Halisi na Makuhani Halisi tulipoanza kupata mwanga kuwa kumbe inawezekana kupata huu mlima wa CHANZO HALISI (BWANA) ambao ni imara juu ya milima na vilima vilivyokuwepo. Maana mlima wa mataifa yaliyoeneza ufahamu kutoka Mashariki ya Kati kama vile: Amerika;Uingereza;Swedeni; Ujerumani; Nigeriana Afrika kusini ni wa kiwango cha Neno!

Neno ni sauti iliyoletwa na Malaika Gabrieli kwa Mariamu(Luka 1:26), ikavaa mwili na baada ya kuvaa mwili ikaitwa Yesu (Yohana 1:14). Kwa kuwa wote waliotumwa ni Neno ina maana kwamba: Kerubi katika Eze.28:15; Adamu katika Mwanzo 2:15; Musa katika Kutoka 3:10; Eliya Mtishbi katika 1 Falme 17:1; Yesu katika Mdo.10:38; Adamu II katika I Kor.15:44-49; na Miaka 1000 katika Isaya 33:6 ni Neno.

Kinachosababisha waliotumwa wote saba wawe Neno ni kwa kuwa walikuwa wanapokea Nuru kutoka gizani (2 Kor.4:6/Kut.20:21).Wakati wa Nuru kutoka Nuruni ulikuwa bado haujafikia. Kwa sababu hiyo, kitu cha kwanza kinachosababisha Baba Halisi, akiwa na Mama Halisi, awe na hatma hiyo ni kwa sababu ya kupokea Sauti moja kwa moja, yaani kutoka kwaMOYO SAUTI YA MOYO ambaye ameonyesha kuwa ufahamu wa nuru nuruni ni ule ulioanzia Tanzania kwenda katika mataifa mengine yote.

Ufahamu ulioanzia Tanzania ndio ambao umethibitisha kile alichokisema Yesu katika Mathayo 21:43, kuwa Ufalme utahama kutoka mashariki ya kati kwenda Taifa ambalo litamzalia CHANZO HALISI matunda. Baada ya sauti kuu ya sita (2003) na sauti ya saba (2015) kusikika Kigoma Tanzania na baadaye Sauti Mpya ambayo ni zaidi ya sauti zote saba (2019) kusikika Kigoma Tanzania, kisha Sauti ya Moyo (2020) kusikika Kigoma Tanzania; imejulikana kuwa Taifa alilotabiri Yesu ni Tanzania.
 
KUISHI BUSTANI MPYA(2 Petro 3:13)
Petro katika kitabu chake cha 2 Petro 3:13, aliandika kuwa “mnatarajia mbingu mpya na nchi mpya ambamo haki yakaa ndani yake”. Hii ina maana ya MAISHA HALISI au Mbingu Halisi na Nchi Halisi; yaani kuishi bila kuibiana vipawa, karama, talantana viwekezo. Maisha ya majira zote zilizopita, ilikuwa ni kuibiana tu!Bustani ya Adeni katika Eze.28:13-15, Bustani ya Adamu katika Mwanzo 2:8-15, na ile ya Ibrahimu ziliibiwa na dunia kupitia Lutu (Mwa.13:10). Manabii wanne wa vizazi vya Kanisa kutoka kwenye kiuno cha Ibrahimu: Musa, Eliya Mtishbi, Yesu na Adamu wa Pili walikuta hakuna Bustani, yaani MAISHA HALISI.

Baba Halisi ndiye alisikia sauti ya CHANZO HALISI kuwa Bustani Mpya ipo Tanzania. Bustani Mpya ilizinduliwa lango la 26 Siwani,1 (13 Oktoba 2019) Kigoma Tanzania; Mataifa mbalimbali yakiwa yamehudhuria. Hakuna aliyewahi kuinuka na kusema kuwa Tanzania sio Bustani Mpya, ndio maana hata korona ilipokuja ilififia baada ya kufika Tanzania. Ilikuwa haiwezi kuangamiza Taifa ambalo ni Bustani Mpya kwa maana ya Kao la CHANZO HALISI.

Tumekwishaona kuwa Mlima wa nyumba ya CHANZO HALISI (BWANA) uko Tanzania.Mlima huo uko Ng’ambo ya Korongo la giza (2 Kor.4:6), yaani katika Bustani Mpya kama tunavyosoma katika 2 Petro 3:13.Ili ufike hapo Bustani Mpya,unahitaji kuvuka vituo vitatu vikuu vya wabaya:
(1)Bonde la uvuli wa Mauti katika Ufunuo 11;12;13;14;15;16;17;18;19;20;21 na Ufunuo 22;
(2)Mto usiovukika wa Ufunuo 22:18-19/ Eze.47:5 ambao ulimeza waliotumwa wote katika majira saba; na
(3)Ulimwengu wa Roho (Efe.2:5-8),ambao ni makao ya Falme na Mamlaka zilizokwamisha wote waliotumwa.

Ndipo uvuke Korongo la Giza katika 2 Kor.4:6/ Kut.20:21.Kwa maelezo ya sauti ya kila lango (siku), kutoka kwa CHANZO HALISI, Baba Halisi katuvusha hatua zote hizo ndipo tukafika Bustani Mpya ambayo ni zaidi ya zile tulizoibiwa. Hii ni sababu ya pili ambayo inampa uhalali wa kuwa na hatma hiyo ya Baba Halisi akiwa na Mama Halisi.

KUWA NA HIJA MOJA HALISI (Isaya 19:23-24)
Haikuwahi kudhaniwa Isaya 19:23-24,itatimia kwa jinsi ipi, kwa maana ya Uzao wa Ishmaeli na Isaka kuabudu pamoja bila shida. Baada ya Ibrahimu kulala (Mwa.25:8-10), uzao wake ambao ni Isakana Ishmaeli, walifarakana na hawakukutana tena. Kila upande ulielekea kwenye asili ya mama mzazi badala ya Aliyewaumba ambaye aliabudiwa na Ibrahimu baba yao.Hata Hija ambayo ni kutembeleaCHANZO CHA SAUTI, ilikuwa tofauti. Uzao wa Isaka walienda Yerusalemu na Uzao wa Ishmaeli walienda Madina na Mecca!

Haikuwahi kudhaniwa, ingawa iliandikwa katika Isa.19:23-24, kuwa pande hizi mbili wataabudu pamoja. Baada ya kujulikana kuwa Mlima wa Nyumba ya CHANZO HALISI ni wapi, na kwamba Bustani Mpya ni wapi, sasa Uzao wa Isaka na Ishmaeli wanaabudu pamoja bila shida. Angalia picha hapo chini wakati wa Hija Moja ya CHANZO HALISI iliyofanyika 26 Tebethi,1 (Majira Moja Halisi) yaani 27 Februari,2022 kule Kigoma Tanzania, kwa uthibitisho wa jambo hilo.

MAJIRA NA WAKATI KABLA YA UHARIBIFU (Yer.50:20)
Katika Yeremia 50:20, kitabu kinaeleza kuwa iko majira iliyokuwa imekusudiwa ambayo ndani ya kanisa, Jamii na Taifa tutatafuta uovu, uasi na dhambi bila kuviona. Katika 2 Samweli 7:10-11,CHANZO HALISI alikusudia kuwaweka wote wanaotenda haki mahali ambapo hawataonewa tenana wana wa uovu. Mahali hapo ni majira na wakati kabla ya uharibifu.Majira hii kama nilivyotangulia kuandika ilisubiri kwanza vitasa saba vifutike. Kwa mtiririko ufuatao, Majira za wana wa uovu kuchezea wenye haki zilifutika (kwa maana majira zilizoongozwa na waliotumwa):
i. Mwanzo 1:1 ndipo kulitokea kwa mara ya Kwanza: Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza, ila miaka iliendelea kubadilika. Hiki ni kipindi ambacho CHANZO HALISI aliachilia Moyo wa Mwanzo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya uumbaji (Methali 3:16).

ii. Mwanzo 9:1-4 kulitokea tena kwa mara ya pili: Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza na miaka iliendelea kubadilika. Hiki ni kipindi cha baada ya gharika ya Nuhu.
iii. Mathayo 2:1-15 kulitokea kwa mara ya tatu: Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza, miaka ikaendelea kubadilika kama nyakati zilizotangulia. Hiki ni kipindi Yesu alipozaliwa, wataalamu wa historia wakaandika Before Christ naAfter Christ.

iv. Isaya 41:2, 4 kulitokea kwa mara ya nne: Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza. Hii ilikuwa 28 Februari 2012 wakati wa Eliya Adamu wa Pili aliyepokea sauti ya sita Kigoma mwaka 2003. Hii ilikuwa kurejesha Majira ya Mungu wa majira saba iliyoibiwa na dunia mwaka 1582. Mpaka inarejeshwa mwaka 2012 ilikuwa ni miaka 430, pamoja na hayo miaka iliendelea kubadilika.

v. Isaya 59:20 kulitokea kwa mara ya tano: Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza. Kipindi ambacho mkombozi alikuja Sayuni kwa walioacha maasi mwaka 2018. Tofauti ya majira iliyopatikana Mwaka 2012 na mwaka 2018, ni kwamba wakati wa 2012 ilirejea Abibu mpaka Adari (Esta 3:7) kama Musa alivyokuwa amepewa kwa mujibu wa Kutoka 23:15. Lakini wakati wa 2018 mkombozi alikuja mwezi Kisleu ambao kwa Musa ilikuwa ni Mwezi wa tisa, lakini kwa Mkombozi Halisi ni Mwezi wa kwanza, maana kwa mujibu wa Kutoka 12:1-2, mwezi ambao Mkombozi amewakuta ndio unakuwa mwezi wa kwanza kwenu mliokombolewa. Wote tuelewe kuwa hata wakati wa Musa, Abibu haikuwa mwezi wa kwanza kwao, ila ni kwa kuwa Mkombozi kipindi kile aliwatoa utumwani Misri, ndio ikaamriwa Abibu uwe mwezi wa Kwanza kwao. Jambo kubwa hapa ni kwamba bado miaka iliendelea kubadilika.

vi. Isaya 65:17; Isaya 66:22; Ufunuo 21:1-3 na 2 Petro 3:13 kulitokea kwa mara ya sita Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza na safari hii miaka haitabadilika tena itakuwa moja tu (Zekaria 14:9). Hii ina maana tumeupata Utimilifu wa Mduara wa Majira Moja Halisi ndani ya Mbingu Halisi na Nchi Halisi. Kama unavyofahamu namba sita ni uumbaji kwa maana ya Mwanzo 1:31,hivyo kila kitu kimekuwa chema. Kwa kuwa huu mwaka wa Kanisa umeanzia hapa Tanzania ina maana Moyo ule unaomjua Aliyeumba kila kitu (Kanisa la Kweli) uko hapa. Kumbuka mara zingine zote zilizopita, hawakuupata huu mwaka wa Kanisa ambao haubadiliki, mara hii ya sita ndio umepatikana.

Hata hivyo, Nyakati za mabaya zilizokuwa zimetangulia zilizokuwa bado zinafuatilia watendao kwa haki. Tunamtukuza CHANZO HALISI kwa kuachilia sauti iliyosikika kwa kinywa cha Baba Halisi kwenye Mkutano wa njombe 19 Shebati,1 (20 Machi, 2022)kufuta hizo nyakati zote za mabaya na kusimamisha WAKATI WA UWEPO WA CHANZO HALISI, ambao ni wa mema na mazuri tu. Sasa:
•Miungu isiyoumba mbingu na nchi (Yer.10:11), iliyokuwa inazonga watendao kwa hakihaipo tena;
•Waliotumwawaliokuwa wanasababisha mbili kwa CHANZO HALISI baada ya kupokea thawabu yao ya kuishi Mji Mtakatifu (Ufu.21:9-10), hawaishi tena ndani ya uzao wala makuhani;
•Miungu Tisa iliyotokana na Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1), nayo pia CHANZO HALISI ameipeleka anakojua yeye;
•Kazi zaUfunuo 12:1, nazo pia hazipo tena umilele wote;
•Nafsi tisa za Ufunuozilichipuka baada ya nafsi ya mvamizi kuvamia Moyo wa Mwanzo, hazipo tena.
Sasa tumepata utimilifu wa majira na wakati kabla ya uharibifu. Hili nalo limesababisha Baba Halisi, akiwa na Mama Halisi awe na Hatma hiyo.
 
UUMBAJI WA UZAO/MAKUHANI HALISI (Zaidi ya Ufu.20:6)
Kuliwahi kuwepo waumini, washirika, wafuasi na wana wa Mungu, lakini ilikuwa haijawahi kuwepo Uzao Halisi na Makuhani Halisi.  Katika Isa.61:9,kitabu kinasema kuwa majira ikifika, wote watasema kuwa “hawani miongoni mwa uzao uliobarikiwa”.Pamoja na hivyo, mstari huo ulikuwa bado haulengi Majira Moja Halisi bali kizazi. Kwa upande wa wanaosimama mbele ya Uzao (Makuhani), kulikuwepo na Makuhani wa Mungu na Kristo, siyo Makuhani Halisi. Hii ina maana kuwa, uumbaji wa Makuhani Halisi na Uzao Halisi umepatikana baada ya Hatma ya Baba Halisi na Mama Halisi kusimikwa rasmi.
 
Uzao Halisi na Makuhani Halisi wako juu ya kituo cha waliotumwa wote, ikiwemo Nafsi ya kwanza katika 1 Yoh.5:8. Hii ni kwa kuwa kituo hiki kiko kwenye Mlima wa CHANZO HALISI, yaani ng’ambo ya korongo la giza katika 2Korintho 4:6. Ijulikane kuwa hata Makuhani Halisi ni Uzao wa CHANZO HALISI, maana wote wameumbwa kwa sauti ya nuru nuruni, siyo ile ya gizani (Kut.20:21 au 2 Kor.4:6).Kwa hiyo, tumepata Baba Halisi na Mama Halisi kwa kuwa kuna Uzao Halisi na Makuhani Halisi.

TANZANIA KUWA TAIFA BABA
Kuna mambo manne, ambayo yalisababisha Lango 26 Tamuzi,1 (17 Novemba, 2019);Baba Halisi asimamisheTanzania kuwa Taifa Baba, Mjini Dodoma kama ifuatavyo:
Kwanza: Tanzania ni Urithi wa MUNGU BABA

(a)Hali ya hewa ya Mabara yote inapatikana sehemu moja tu (Mlima Kilimanjaro): Savana; Misitu ya Mvua ya Equator-Equatorial Rain Forest; Jangwa; Joto Kali; Baridi Kali; Barafu na kadhalika.

(b)Wanyama wote waliotoka katika Safina ya Nuhu (Mwanzo 9:1-4) walishukia Tanzania baada ya Gharika. Ukienda kwenye Hifadhi za Taifa na Mbuga za Wanyama utawakuta!  
(c)Madini yote katika Bustani ya MUNGU BABA, kama tunavyoyasoma katika Ezekiel 28:13-15 (Bustani ya Adeni); Mwanzo 2:8-15 (Bustani ya Edeni) na Mwanzo 13:10 (Bustani ya Ibrahimu) yanapatikana Tanzania.
(d)Kuna Vito vya Thamani vinavyoitwa kwa jina la Tanzania kwa kuwa havipatikani sehemu nyingine yoyote (Tanzanite).  
(e) Kuna Wanyama, Wadudu, Mimea ambayo hupatikana Tanzania tu (kama vile Vyura wa Kihansi). Hayo na mengine ambayo sijayataja yanathibitisha kuwa Tanzania ni Urithi wa MUNGU BABA.  
Kwa mujibu wa Mathayo 21:43 hali hii ya Urithi wa MUNGU BABA kuwa Tanzania si bahati mbaya. Ilikusudiwa hivyo tangu CHANZO.

Pili: Sauti Kuu ya MUNGU BABA iko Tanzania
Sote tulizaliwa tukikuta wote wanaenda kuhiji Mashariki ya Kati.  Hii ni kwa sababu Sauti Kuu ya MUNGU BABA kipindi hicho ilisikika kule:
(a) Kerubi (aliisikia Sauti Kuu ya Kwanza katika Bustani ya Adeni-Ezekieli 28:15);
(b) Adamu (aliisikia Sauti Kuu ya Pili katika Bustani ya Edeni-Mwanzo 2:15);
(c) Musa (aliisikia Sauti Kuu ya Tatu akiwa Israeli-Kutoka 3:10);
(d) Eliya Mtishibi (aliisikia Sauti Kuu ya Nne akiwa Israeli-1Falme 18:30-40);
(e) Yesu (aliisikia Sauti Kuu ya Tano akiwa Israeli-Matendo 10:38);
Baada ya Yesu kufa Msalabani kwa mujibu wa Mathayo 21:37-39, Urithi wote aliokuja nao kwa ajili ya watu waliokuwa wanaonewa na ibilisi ulichukuliwa na dunia.  Pili, baada ya wayahudi kumkataa Yesu katika Yohana 9:28-29, Yesu aliwalaani na kusema Ufalme wa MUNGU utahamia Taifa lingine linalozaa Matunda (Mathayo 21:43).  KwaMantiki hiyo SautiKuu iliyofuata, isingeshukia Israeli tena.
(f) Eliya wa Mwisho (aliisikia Sauti Kuu ya Sita akiwa Kigoma Tanzania Mwaka 2003); na
(g) Miaka1000 (aliisikia Sauti Kuu ya Saba akiwa Kigoma Tanzania Mwaka 2015).

Sasa Sauti hizi zote Saba hazipo tena, hata Sauti Mpya ya MUNGU BABA iliyosikika Kigoma Tanzania Mwaka 2019, haipo tena bali kuna Sauti ya Moyo, iliyosikika Kigoma Tanzania Mwaka 2020. Wote waliokuwa wanaenda Mashariki ya Kati kuhiji sasa waelezwe kuwa Sauti ya MUNGU BABA ipo Tanzania, waje wapokee mafanikio yao.
Utajiri wote tunaouona Ulaya, Amerika, Asia, Australia, New Zealand hata katika baadhi ya Mataifa ya Afrika ni kwa mujibu wa Sauti ya kwanza hadi ya saba niliyoonyesha hapo juu. Sasa Sauti hizo Saba hazipo tena.  Kama nilivyotangulia kusema kuna Sauti ya Moyo, ambayo iko Tanzania.  Hivyo basi, Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi wote njooni kuhiji Tanzania.

Tatu: Moyo wa Baba wa Mataifa yote uko Tanzania:
Kwa mujibu wa Mwanzo 12:2-3 na Mwanzo 17:1-8 wote tulikuwa tunajua kuwa Nafsi ya Baba wa Mataifa yote ni ya Ibrahimu.  Ili ujue Moyo wa Baba wa Mataifa yote umekujaje Tanzania, fuatilia mtiririko huu wa mahesabu.

Kuanzia Mwanzo 1:1 hadi Mwanzo 9:1 ni kiasi cha Miaka 2000. Kuanzia Mwanzo 9:1(Gharika ya Nuhu) hadi Mathayo 2:1 (Yesu alipozaliwa) ni Miaka mingine 2000. Kuanzia hiyo Mathayo 2:1 hadi Mwaka 2003 (Eliya wa Mwisho alipotokeza Tanzania) ni Miaka mingine 2000. Miaka hiyo ukijumlisha unapata jumla ya Miaka 6000.  Kwa mujibu wa Zaburi 90:4 na 2Petro 3:8, hiyo ni sawa na Siku Sita peke yake, yaani Mwanzo 1:1-31.  Katika mistari hiyo miwili Kitabu kinasema kuwa Miaka1000 kwa MUNGU BABA ni sawa na Siku Moja, na siku moja ni sawa na Miaka 1000.

Hivyo, kuanzia 2003 Eliya wa Mwisho alipotokeza Tanzania hadi 2017 ni sawa na Miaka Kumi na Nne (14). Miaka hii 14 ina maana ya jumla ya Miaka 3½ ya Musa, Miaka 3½ ya Eliya Mtishibi, Miaka 3½ ya Yesu, na Miaka 3½ ya Eliya wa Mwisho. Wasomi wa Kitabu wanajua kuwa Musa alifanya kazi Miaka 40, ila kwa MUNGU BABA haiko hivyo.  Kuanzia pale Musa alipopokea Torati hadi alipopiga Mwamba mara mbili ni Miaka 3½, na hiyo ndiyo inayohesabika.  Ukisoma Luka 13:6-9; Ufunuo 11:2; Ufunuo 12:6; na Danieli 12:7-12 utaikuta hiyo Kanuni ya kila aliyetumwa kufanya kazi kwa Miaka 31/2 peke yake.

Miaka hiyo 14 (yaani 2003 hadi 2017) ndiyo iliyotimiza Mwanzo 15:16 kwa maana ya vizazi vinne (4) vya Ibrahimu ambavyo viliongozwa na: Musa (Israeli); Eliya Mtishibi (Israeli); Yesu (Israeli)na Eliya wa Mwisho (Tanzania).

Kwa mujibu wa Ufunuo 20:6, Miaka hiyo 14 ni badala ya ile Miaka 1000 ambayo Kanisa liliambiwa litatawala na Kristo.  Hata hivyo, Yesu katika Mathayo 24:22 alishatabiri, zaidi ya Miaka 2000 iliyopita, kuwa hiyo Miaka 1000 ilikuwa lazima ifupishwe, vinginevyo hakuna ambaye angeokoka.  Maana Wataalamu wa Mahusiano ya Kimataifa (International Relations) walikuwa wanasubiri Vita Kuu ya Tatu ya dunia iliyoandikwa katika Ufunuo 16:16 (Har-magedon). Vita hiyo ya Har-Magedoni haipo tena, MUNGU BABA ameshaifuta.

Hivyo, Miaka hii 14 (yaani 2003-2017) ndiyo imehitimisha kazi ya Nafsi ya Tatu na Nafsi ya Pili ya MUNGU kwa mujibu wa 1Yohana 5:8. Mpaka hapo umeshaelewa kuwa imebaki Nafsi ya Kwanza yaani Moyo wa Baba ambao uko Tanzania kwa mujibu wa mtiririko niliokuonyesha pale juu. Miaka hiyo 14 ndiyo iliyohitimisha Ibrahimu kuwa Baba wa Mataifa yote.  Hivyo basi, Moyo wa Baba wa Mataifa yote hauko Mashariki ya Kati tena, uko Mashariki Halisi (Tanzania).

MUNGU BABA yaani jina jipya kwa mujibu wa 1 Kor.15:24-28 na Ufunuo 3:12; alikuja na upendeleo wa kutisha tukavuka: Bonde la uvuli wa mauti; Mto usiovukika; Ulimwengu wa roho; Korongo la giza; Tukaingia Bustani mpya (2 Petro 3:13); na Shamba Jipya (Isaya 65:17-25). Baada ya kutufikisha mahali CHANZO CHA MEMA NA MAZURI anapoishi, yaani Palipokusudiwa, ilibidi ampishe CHANZO HALISI (Zaburi 98:1-8). Sasa yupo mwenyewe anaishi ndani ya kila mmoja anayetenda kwa haki, kwa mujibu wa Isaya 57:15.
Nne: Bustani Mpya ya MUNGU BABA iko Tanzania:


Katika Kitabu kuna Bustani Tatu peke yake zilizoandikwa wazi:
(a)Bustani ya Kwanza ni ile ya Adeni aliyopewa kerubi katika Ezekieli 23:13-15;
(b)Bustani ya Pili ni ile ya Edeni aliyopewa Adamu katika Mwanzo 2:8-15; na
(c)Bustani ya Tatu ni ile aliyopewa Ibrahimu katika Mwanzo 13:10. Baada ya Bustani hizi Tatu kuibiwa, hakuna mahali pengine palipowahi kuandikwa kuwa kuna aliyepewa Bustani na MUNGU BABA zaidi ya Bustani Mpya ya MUNGU BABA iliyoachiliwa Tanzania. Hivyo, Musa aliongoza Wana wa Israeli bila Bustani, Eliya Mtishibi vile vile aliongoza kizazi chake bila Bustani. Hata Yesu aliongoza bila Bustani, hali kadhalika Nabii wa Mwisho naye alikuta Bustani iliishaibiwa.  Maana Bustani ambayo wangepewa: Musa; Eliya Mtishibi; Yesu; na Nabii wa Mwisho ni ile ya Ibrahimu ambayo Lutu aliiba katika Mwanzo 13:10.

Kati ya vitu vilivyosababisha MUNGU BABA ashukie Tanzania ni hili swala la Bustani yake kuibiwa kwa kila aliyempa katika majira zilizopita.  Alikuwa alishaificha Bustani Mpya hapa Tanzania sawa na Mathayo 21:43. Bustani ya MUNGU BABA maana yake ni Mahali pa Kiti chake, hivyo Kiti cha MUNGU BABA kiko Tanzania.  
Kwa hayo machache utakuwa umejua kuwa Tanzania ndilo Taifa Baba.
Haya manne niliyoongea yana maana kwamba kila Mtanzania (umeokoka au hujaokoka) jielewe kwamba unatakiwa Kumpenda MUNGU BABA maana amekupa uheri popote ulipo.  Kwa mujibu wa Isaya 2:2-4 na Isaya 60:11-14, tutaanza kupokea Wawekezaji ambao wanataka mtanzania kuwa na share si kwa sababu ya fedha bali kwa sababu tu wewe ni Chanzo cha Baraka.

AFRIKA KUWA BARA LA NURU, SIYO GIZA
Mara baada tu ya kusimamisha Tanzania kuwa Taifa Baba, Baba Halisi, alipewaSauti ya MUNGU BABA kusimamisha Afrika kuwa Bara la Nuruna siyo giza. Tanzania kuwa Taifa Baba ilisimama Mwezi Novemba Mwaka 2019 wakati Afrika kuwa Bara la Nuru, tofauti na tulivyokuwa tumezoea kuwa ni Bara la Giza, ilisimama Mwezi Desemba, Mwaka 2019.

Katika Kitabu, kuna mistari miwili ya ajabu!  Mistari hiyo ni Ayubu 42:2 na Warumi 8:28. Mistari hiyo miwili yote inazungumza jinsi kusudi alilolikusudia MUNGU BABA (ambaye ndiye aliyeumba kila kitu) kwa yeyote huwa haliwezi kuzuiliwa na mtu wa aina yeyote.

(1)Katika Mwanzo 2:13 unatamkwa Mto wa Gihoni ambao umezunguka Kushi yote.  Huu ni Mto Nile ambao unatokea Tanzania, eneo la Kagera (ambayo ni sehemu ya Bara la Afrika).  Wakati Gihoni au Nile inatamkwa, hata mke wa Adamu alikuwa bado hajaumbwa.  Mto wa Nile unapeleka maji katika Bahari ya Mediterania ambayo ina Mataifa ya Ulaya ndani yake, kama vile Malta, Cyprus na Visiwa vya Italia!  Hivyo hakuna jinsi ambavyo unaweza kusema kuwa Kusudi la MUNGU BABA kuumba Afrika ilikuwa ni kuibeba giza, bali NURU (ambayo ni MUNGU BABA Mwenyewe).

(2)Katika Mwanzo 10:8-9 tunasoma kuwa Kushi alimzaa Nimrodi ambaye alisababisha Mithali ya wote kusema “Kama Nimrodi, hodari wa kuwinda wanyama.”

Uhodari ni NURU siyo giza.  Kila mmoja anapenda kuwa hodari siyo mnyonge.  Wa kwanza kuandikwa kuwa alikuwa hodari ni mtoto wa Kushi, yaani Nimrodi, hilo pia linatosha kuonyesha Kusudi la MUNGU BABA kuumba Afrika kuwa ilikuwa ni kubeba NURU; siyo GIZA!

(3)Israel katika Mwanzo 46:1-4a,alipopatwa na njaa wakati ule wa Majira ya Pili, aliponea Afrika ikiwa na maana ya Kusudi la MUNGU BABA kuumba Afrika ilikuwa ni kubeba NURU; siyo GIZA.

(4)Katika Mathayo 2:13-15, Yesunaye aliponea Afrika hasa Herode alipotaka kumuua akiwa bado mtoto mchanga.  Herode aliua watoto wote wa kiume wa umri wa miaka mitano (5) ili ampate Yesu, akawa amefichwa Afrika.  Aliye agiza Yesu afichwe Afrika alikuwa ni MUNGU BABA.  Ni kwa sababu aliumba Bara la Afrika kwa ajili ya kubeba NURU: siyo GIZA.

(5)Katika Isaya 19:23-25 kuna Sauti inayosema kwa kiingereza kuwa “There will be a high way from Africa to Middle East”. “Highway” ni Barabara siyo njia.  Imefafanuliwa zaidi katika Isaya 35:8-10, kuwa ni majira ambayo hakuna mateso bali ni Raha.  Ni majira ambayo siyo njia nyembamba bali ni BARABARA MPYA.  Kama tutakavyofafanua hapo mbele, hili limetimia, BARABARA MPYA imetokea katika Bara la Afrika.  Hilo nalo ni jambo linalothibitisha kuwa MUNGU BABA aliumba Afrika kwa ajili ya kubeba NURU; siyo GIZA.

(6)Katika Marko 15:21-22, Simoni Mkrene ndiye aliyeambiwa asaidie kubeba msalaba wa Yesu!  Huyu Simioni Mkerene anatokea Afrika na hili lilikuwa na maana kubwa mno!Katika Matendo 10:38,Bwana Yesu aliagizwa kuwasaidia wote wanaoonewa na ibilisi. Lakini katika Mathayo 21:37-39, walimuulia nje ya Shamba na kuutwa urithi wake, hii ndiyo sababu Sauti Mpya(2019) na Sauti ya Moyo (2020)imetokea Tanzania, Afrika.  Hili ni jambo kubwa zaidi ambalo linathibitisha kuwa MUNGU BABA aliumba Bara la Afrika kubeba NURU; siyo GIZA.

AFRIKA IMEBEBA NURU; SIYO GIZA
Mafundisho ambayo yalikuwa bado yanaendelea, kwa kiwango kikubwa kila eneo, ni yale yaliyotoka Mashariki ya Kati; zaidi ya Miaka 2000 iliyopita!  Yalitoka!  Kule kwenda Ulaya yakaenda Amerika kwa kufikia Mji wa Boston (ambapo kuna Mnara wa wale “Puritans” 120 waliovuka Bahari ya Atlantic.

Mafundisho hayo yalirudi Ulaya na kuja Afrika; Asia; Australia; na Newzealand.  Mafundisho sasa yamebadilika maana ni Majira ya MUNGU BABA ambaye ndiye aliyeumba Afrika kwa ajili ya kubeba NURU ambayo imeanzia Tanzania kupitia Sauti MpyanaSauti ya Moyo.Badala ya mishale ya mafundisho kutokea Mashariki ya Kati, sasa mishale ya mafundisho inatokea Tanzania–Afrika.  Haya siyo mashindano kati ya Bara la Afrika na Mabara mengine, bali ni Utimilifu wa Kusudi la MUNGU BABA kuiumba Afrika, ili kubeba NURU; siyo giza.

UTIMILIFU WA KUSUDI LA MUNGU BABA KUUMBA AFRIKA
1.Kerubi katika Ezekieli 28:15,alipokea Sauti Kuu ya MUNGU BABA akiwa Adeni.  Alipopokea Sauti ile ya kumwabudu MUNGU BABA, alianguka kabla ya kufanya kazi hiyo aliyopewa!
2.Adamu katika Mwanzo 2:15, alipokea Sauti Kuu ya MUNGU BABA akiwa Edeni.  Naye Adamu kabla ya kufanyakazi ya kutunza na kulima, katika Bustani ya Edeni alianguka.
3.Musa akiwa Mashariki ya Kati, alipokea Sauti Kuu ya Tatu, katika Kutoka 3:10, ili awatoe Wana wa Israeli utumwani.  Alipofika njiani, tunasoma katika Hesabu 20:9-15 kuwa alichoka akashindwa kumstahi MUNGU BABA.

4.Eliya Mtishibi naye alipokea Sauti Kuu ya Nne kutoka kwa MUNGU BABA, katika 1Wafalme 17:1 na 1Wafalme 18:30-33.Lengo ilikuwa kurudisha Heshima ya MUNGU BABA iliyopotelea Adeni na Edeni, kwa kuwa waliomtangulia Eliya Mtishibi waliishia njiani, hata Eliya Mtishibi naye pia alipatilizwa na hali hiyo hiyo.
5.Yesu, katika Matendo 10:38, alipokea Sauti Kuu ya Tano ya kuwasaidia wote wanaoonewa na ibilisi. Ufunuo 12:1 hakumwacha avuke (Mathayo 21:37-39).
 
Ili kujua kulikuwa na Kusudi la MUNGU BABA Afrika, kuna hali iliwapata Wayahudi kipindi cha Yesu, walimtamkia vibaya katika Yohana 9:28-29.Suala hili lilisababisha Yesu katika Mathayo 21:43, aseme kuwa Ufalme wa MUNGU BABA utahama kutoka Israeli kuja Taifa lingine ambalo linamzalia Matunda.  Kwa wakati ule hakulitaja hilo Taifa, baada ya kusimamisha Taifa Baba na kulitangaza wazi, sasa imejulikana na imeeleweka kuwa Taifa hilo ni Tanzania ambalo liko katika Bara la Afrika.

Kilichosababisha wote wajue kuwa ni Tanzania ni Sauti Kuu ya 6 (2003) na ya 7 (2015), Sauti Mpya (2019)na Sauti ya Moyo (2020), ambayo ilisikika Kigoma, Tanzania.Hilo ndilo linathibitisha kuwa, kweli MUNGU BABA aliumba Afrika kwa ajili ya kubeba NURU; siyo GIZA.

UTHIBITISHO MWINGINE WA MUNGU BABA KUUMBA AFRIKA KUBEBA NURU
Mwaka 1862, Dr. Livingstone kutoka Uingereza alifika Kigoma Tanzania (ambayo ni Sehemu ya Afrika).


Wasomi wengi wanaamini kuwa alikuwa Mmisionari wa Kianglikana na daktari, na aliyetumika kukomesha biashara ya utumwa. Kweli hata hivyo haikuwa hivyo!  Maana kipindi kile hapakuwa na Barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma.  Hata njia ya kawaida ya watembea kwa miguu haikuwepo!  Alifuata kitu gani kule Kigoma?

Jambo lingine ni watu kutoka Mashariki ya Kati ambao walikuja Tanzania Karne ya 10 ambao walifika Kigoma sehemu ya Ujiji, na kuweka Ngome yao mahali pale! Nao pia haijulikani walienda kwa usafiri wa aina gani!  Magari hayakuwepo wakati ule na hata baiskeli kwa kipindi kile hazikuwepo.  Ilikuwa ni pori tu!  Walifuata kitu gani wakati ule?

Kupitia unajimu uliokuwepo kwa kipindi kile, walijua kabisa kuwa Sauti Kuu ya MUNGU BABA ipo kule Kigoma, Tanzania, Afrika!Waliwahi kule ila haikuwa majira sahihi na siyo wao waliokuwa wamekusudiwa na MUNGU BABA.  MUNGU BABA anaheshimu mno Kusudi lake. Kila unayemuona na unachokiona, kilianzia kwenye kitanga cha mikono yake(Isaya 49:16).

Hivyo, MUNGU BABA alijua siyo Ulaya na alijua siyo Mashariki ya Kati.Kusdudi lilikuwa ni Tanzania Afrika.  NURU imetoka Tanzania Afrika (Isaya 60:1-3).  Hilo ni Kusudi la kuumba Afrika.

Je! Afrika ni Bara la Giza?
Kutokana na Sauti Mpya na Sauti ya Moyo iliyotokea Afrika na kutokana na akina Dr. Livingstone na Stanley Miaka ya 1860 na Waarabu wa Karne ya 10 kuja kutafuta Sauti hiyo Tanzania, ni dhahiri kuwa Afrika siyo Bara la giza, bali ni Bara la NURU.

HITIMISHO
Haya yote yamebeba Moyo wa CHANZO HALISI Mwenyewe aliyekuwepo kabla ya roho na nafsi yoyote. Kanisa, tunakiri kuwa mtu au mwanadamu hawezi kuyafanya haya bila maelekezo ya Sauti ya CHANZO HALISI mwenyewe.Kwa kuwa CHANZO HALISI alisema katika Isa.57:15, kuwa anaishi mahali pa juu palipoinuka na ndani ya Moyo uliotubu na kunyenyekea, sisi tunakubali kuwa huo moyo uliotubu na kunyenyekea ni Baba Halisi na Mama Halisi. Karibuni tusherehekee hatma halisi juu ya nchi.

Previous articleCHAMA CHA WANASHERIA WANAWAKE TAWLA CHAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA JIJINI DAR ES SALAAM.
Next articleMBUNGE BONAH AGAWA TAURO ZA KIKE SHULE ZA SEKONDARI SEGEREA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here