Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu akizungumza alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya siku tano ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Wizara hiyo na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar katika kuandaa na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo. mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wamikutano wa TBS kuanzia April 11,2022 Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi sera na Mipango Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Julieth Magambo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mratibu wa Mradi huo Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Natasha Ngowi akiielezea umuhimu wa mafunzo hayo katika kutafasiri vema mipango ya maendeleo ya kitaifa alipokuwa akitoa hotuba yake ya utangulizi
Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanziba Bi. Nana Mwanjisiakitoa salamu zake kwa upande wa Visiwani Zanzibar katika mafunzo hayo.
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu amewataka Maafisa wanaoshiriki mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo katika kuandaa na kusimamia miradi ya maendeleo, kuyatumia vema mafunzo hayo ili kuleta tija pindi watakapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo April 11,2022 Jijini dar es Salaam alipokuwa akizungumza wakati wa kufungua rasmi mafunzo hayo kwa Maafisa wa Wizara na Taasisi husika wakiwemo washiriki kutoka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kupitia Mradi wa EIF TIER II unaolenga kuwajengea uwezo maafisa hao.
Ameeleza kuwa ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo utachochea shughuli zote za kiuchumi zinazohusiana na sekta hizo kutokana na uwepo wa Miradi hasa kwenye sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara itakayopelekea nchi kufikia katika Dira ya Maendeleo yam mwaka 2055 ya uchumi wa viwanda.
“Natarajia katika mafunzo haya mtaitumia fursa hii hadhimu iliyotolewa chini ya Mradi huu wa EIF TIER II kujifunza kwa bidii ili kutimiza lengo la mradi na nchi katika kuleta maendeleo na baada ya mafunzo haya mtaweza kuandaa na kusimamia vema miradi ya maendeleo inayohusiana na sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na kuwa na uwezo wa kufanya tathimini ya miradi hiyo” Amesema Gugu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi sera na Mipango Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Julieth Magambo amesema kuwa uwepo wa mafunzo hayo kutachochea katika kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwenye miradi mbalimbali kwa kufanya uwekezaji na kuendeleza biashara hapa nchini.
“Pia kuwepo kwa mafunzo haya kutawezesha kuandaa miradi ya kuimarisha soko na kukuza Biashara na hivyo itakuwa ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi”ameeleza Magambo.
Naye Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanziba Bi. Nana Mwanjisi amesema kuwa ana matumaini makubwa na mafunzo hayo yatakwenda kuwaongezea ufansi hasa katika maeneo ya utafiti utakaopelekea kukuza uzalishaji katika maeneo ya kimkakati ya Biasahara na uwekezaji
Awali akizungumza alipokuwa akitoa hotuba ya utangulizi juu ya mradi huo Kaimu Mratibu wa Mradi huo Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Natasha Ngowi ameeleza umuhimu wa mafunzo hayo katika kutafasiri vema mipango ya maendeleo ya kitaifa katika kila hatua ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuhamasisha matumizi ya rasilimali.
“Nimatarajio yangu kuwa baada ya mafunzo haya maafisa mnaoshiriki mafunzo haya mtaweza kuandaa miradi ya kimaendeleo yenye tija itakayotekeleza mipango ya sekta za Uwekezaji, Viwanda na Biashara”amesema Natasha.
Mafunzo hayo ya siku tano yanayoendelea katika Ukumbi wa mikutano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) yamwakutanisha jumla ya washiriki 30 kutoka kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na yanaongozwa na wawezeshaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.