Waogeleaji wa Tanzania, makocha na viongozi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Julius Nyerere (Terminal -3). Waogeleaji hao walishiriki katika mashindano ya kanda ya nne ya Afrika nchini Zambia na kushinda medali 13.
………………………………………….
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) na Chama Cha Kuogelea (TSA) zimewapongeza timu ya Taifa ya mchezo wa kuogelea wa Tanzania kwa matokeo mazuri waliyopata katika mashindano aya kana ya Nne Afrika yaliyomalizika hivi karibuni mjini, Lusaka, Zambia.
Tanzania iliwakilishwa na jumla ya waogeleaji 18 katika mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi nyingine 13. Waogeleaji wa Tanzania walishinda jumla ya medali 13 ambapo nne za dhahabu, nne za Fedha na tano za Shaba.
Muogeleaji chipukizi Filbertha Demello (12) ameshinda jumla ya medali sita, ikiwa tatu za dhahabu, moja fedha na mbili za shaba.
Filbertha ambaye anatokea klabu ya Bluefins, pia ameshinda kikombe cha mshindi wa tatu kwa waogeleaji wenye umri wa miaka 12. Nahodha wa timu hiyo, Collins Saliboko ambaye anatokea klabu ya Dar Swim Club (DSC) alishinda medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na mbili za dhahabu.
Muogekeaji mwingine Mark Tibazarwa wa DSC alishinda medali tatu ambapo mbili za fedha na moja ni shaba.
Mbali ya kushinda medali, waogeleaji wa Tanzania pia waliweza kuhimarisha muda (PBs) katika mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi nyingine 13. Waogeleaji wengine wa Tanzania walioshiriki katika mashindano hayo ni Julius Missokia, Mischa Ngoshani, Mahek Desai, Michael Joseph, Austin Okore, Sarah Tibazarwa na Salman Yasser.
Wengine ni Muskan Gaikwad, Isaac Mukani, Aminaz Kachra, Lina Goyayi, Enrico Barretto, Maryam Ipilinga, Delbert Ipilinga na Ethan Alimanya.
Afisa michezo wa Baraza la michezo Tanzania (BMT), Halima Bushiri alisema kuwa waogeleaji hao wameweza kuitangaza vyema nchi nje ya mipaka yake na kuleta heshima katika mashindano ambayo Tanzania ilialikwa. Tanzania ilikusanya jumla ya pointi 902 na kushika nafasi ya tisa.
“Matokeo yametufanya kujivunia kwani Tanzania iliwakilishwa na waogeleaji chipukizi ambao wamewezakufanya vyema pamoja na kuwa na umri mdogo. Hii ni ishara kuwa mchezo wa kuogelea unazidi kupata maendeleo na mafanikio,” alisema Halima.
Mwenyekiti wa TSA, Imani Alimanya pia aliwapongeza waogeaji hao kwa matokeo na kushinda medali huku wengine wakiweka muda mpya.
Alimanya alisema kuwa wanaamini kuwa muda si mrefu, waogeleaji wa Tanzania wataweza kufanya vyema katika mashindano ya Dunia, Olimpiki na Jumuiya ya Madola.