Morogoro
Wizara ya Madini imeanza zoezi la kuandaa Mpango Mkakati mpya (Strategic Plan) wa miaka mitano (2026/27–2030/31) utakaotoa mwelekeo mpya wa maendeleo ya Sekta ya Madini nchini, baada ya kukamilika kwa mapitio ya Mpango Mkakati unaomaliza muda wake.
Kikao kazi hicho kinachofanyika mjini Morogoro kimewakutanisha Wataalamu wa Wizarani na taasisi zilizo chini ya Wizara ambazo ni Tume ya Madini, Taasisi ya Jilojia na Utafiti wa Madini (GST), Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI, Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Pamoja na wadau wengine muhimu akiwemo mtaalam mwelekezi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), kwa kufuata mwongozo wa uandaaji wa Mpango Mkakati wa kisekta ulioandaliwa na NPC kwa kutumia tathmini ya utekelezaji wa mpango uliopita uliotumika kubaini changamoto na kuweka vipaumbele vipya vitakavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na maelekezo ya viongozi wa kitaifa.
Akizungumza katika Kikao hicho, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini, Augustine Ollal, amesema Mpango Mkakati mpya unapaswa kuwa chombo madhubuti cha kuleta mageuzi ya kweli katika usimamizi na maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.
“Mpango huu mpya lazima ujibu mahitaji ya wakati huu tulionao. Tunataka kuona Sekta ya Madini ikiendelea kuwa nguzo imara ya uchumi wa taifa, ikiongeza mapato ya Serikali, ajira kwa Watanzania, kuendelea kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa viwanda kupitia uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi, huo ndio mwelekeo wetu mpya” amesema Ollal.
Ameongeza kuwa maandalizi ya mpango huo yatazingatia uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa mpango uliopita pamoja na mabadiliko ya kimkakati yanayotokea katika Sekta ya Madini ulimwenguni hivi sasa.
“Sote tunafahamu kuwa, Dunia inaelekea kwenye matumizi nishati safi na teknolojia mpya zinazotegemea madini mkakati. Hivyo, mpango wetu lazima uweke mkazo kwenye usimamizi endelevu wa rasilimali zetu, matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, na ushirikishwaji mpana wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani ya madini,” amesisitiza Ollal.
Mkurugenzi Ollal amebainisha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kinachomalizika ikiwemo ongezeko la Mapato ya Serikali, kufikia lengo la uchangiaji wa sekta katika Pato la Taifa GPD kabla ya wakati uliopangwa, kuimarika kwa usimamizi wa wachimbaji wadogo na kuongezeka kwa uwekezaji, bado kuna haja ya kuongeza nguvu katika maeneo ya urasimishaji, afya na usalama migodini.
Washiriki wa kikao hicho wameeleza kuwa Mpango Mkakati unaoandaliwa utaweka malengo yanayopimika, viashiria vya utekelezaji na mikakati itakayohakikisha Sekta ya Madini inachangia zaidi katika ukuaji wa uchumi jumuishi na kuendelea kuwa sekta fungamanishi.





