Home INTERNATIONAL WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CHINA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA...

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CHINA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KIKAZI

 

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Wang Yi, amewasili Dar es Salaam, Tanzania, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 9 hadi 10 Januari 2026.

Katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Mheshimiwa Wang Yi amelakiwa na mwenyeji wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), Naibu Mwaziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na Mhe. James Milya, Katibu Mkuu Balozi Dkt Samwel Shelukindo na viongozi wengine wa Serikali

Ziara hiyo inalenga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China.

Ziara hiyo pia inalenga kukuza ushirikiano kwa kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na kuangazia fursa mpya za ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.

Akiwa nchini Mheshimiwa Wang Yi atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshiniwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo ambayo yatalenga kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China

Mheshimiwa Wang Yi pia atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaaam ambako pia atawasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping

Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, ambapo kwa mwaka 2024 thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 5.2. Kampuni za China pia zimeendelea kuwekeza nchini.

katika sekta za viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii. Kwa mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili miradi ya China 343 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1 na kuzalisha ajira 82,404.

Tanzania na China pia zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya miundombinu ya uchukuzi ambapo reli ya TAZARA ni moja wapo ya alama ya urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. Reli hiyo ina urefu wa Kilomita 1860 ambapo, kilomita 975 zipo Tanzania na kiliomita 885 zipo Zambia, na imebaki kuwa kielelezo cha kihistoria cha uhusiano wa karibu uliojengwa kwa misingi ya umoja, mshikamano na udugu kati ya Tanzania na China.

Aidha, ziara hii ni kielelezo cha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China ambao umejengwa kwenye misingi ya kuaminiana na kuheshimiana ukiwa umedumu kwa zaidi ya miongo sita. Msingi wa ushirikiano huo uliwekwa na waasisi wa mataifa haya, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, ambao unaendelea kuenziwa kwa vitendo na viongozi wa mataifa haya.