Home INTERNATIONAL WATALII 85 KUTOKA MATAIFA SITA WATEMBELEA MAGOFU YA KILWA

WATALII 85 KUTOKA MATAIFA SITA WATEMBELEA MAGOFU YA KILWA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi wetu, Kilwa – Lindi.

Tanzania imeendelea kuthibitisha kuwa ni kisiwa cha amani na kivutio kikubwa cha utalii duniani, baada ya meli ya kitalii Island Sky Nassau kutia nanga leo tarehe 15 Januari 2026 katika Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya Usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, ikiwa na jumla ya watalii 85 kutoka mataifa mbalimbali ya dunia.

Watalii hao wametoka katika nchi za Australia, Finland, Ujerumani, Ireland, Netherlands na Uingereza, hali inayoonesha imani kubwa ya jumuiya ya kimataifa kwa usalama, amani na ukarimu wa Tanzania.

Ziara hiyo imeratibiwa na kampuni ya Takims Holidays Tours & Safaris Ltd, ambayo imeendelea kuwa mdau muhimu katika kukuza utalii wa kimataifa, hususan utalii wa kihistoria na utamaduni katika maeneo ya Urithi wa Dunia
.
Akizungumza baada ya mapokezi ya wageni hao,.Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja alisema kuwa ujio wa watalii hao ni ushahidi tosha kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, tulivu na yenye mazingira rafiki kwa wageni, licha ya changamoto mbalimbali zinazoikumba dunia.

“Hifadhi yetu imeendelea kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani. Mwaka jana tulipokea meli 9 zikiwa na jumla ya watalii takribani 1, 130. Na kwa mwaka huu hii ni meli ya kwanza ambapo mwezi huu wa Januari tunatarajia kupokea meli zingine zaidi ya 3 zikiwa zimesheheni watalii na nyingine nyingi kuendelea kuja ” alisema Maganja

“Huu ni uthibitisho kuwa Taifa letu Tanzania bado ni Kinara wa amani ndio maana mataifa mbalimbali bado yanaendelea kuvutiwa kutembelea vivutio vyake” alisisitiza

Hifadhi ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, ambayo ni urithi wa dunia chini ya UNESCO, inaendelea kuvutia wageni kutokana na historia yake ya kipekee ya biashara ya kale ya Bahari ya Hindi, usanifu wa majengo ya mawe na mchango wake mkubwa katika historia ya Afrika Mashariki.

Ujio wa meli ya Island Sky Nassau unaongeza thamani katika juhudi za serikali na wadau wa utalii za kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii, huku ukitangaza ujumbe muhimu kwa dunia kuwa Tanzania bado ni kisiwa cha amani, mshikamano na ukarimu, ndicho kinachoifanya iendelee kupokea wageni wengi kutoka pembe zote za dunia.