Home LOCAL USHIRIKISHWAJI WA JAMII NI NGUZO MUHIMU YA UTUNZAJI WA RASILIMALI ZA BAHARI

USHIRIKISHWAJI WA JAMII NI NGUZO MUHIMU YA UTUNZAJI WA RASILIMALI ZA BAHARI

http://USHIRIKISHWAJI WA JAMII NI NGUZO MUHIMU YA UTUNZAJI WA RASILIMALI ZA BAHARI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mwamvua Mwinyi, Mafia

January 1,2026

Ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa mazingira, hususan rasilimali za bahari, umetajwa kuwa nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, hususan katika kukuza uchumi wa buluu unaolenga kunufaisha wananchi moja kwa moja.

Katika kutekeleza azma hiyo, Shirika la WATONET limezindua mradi wa Uimarishaji wa Vikundi Shirikishi vya Usimamizi wa Rasilimali za Bahari na Pwani (BMU na VLC), utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2026 hadi 2028.

Akizindua mradi huo , Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, aliwataka watekelezaji wa mradi huo kujikita zaidi katika utendaji unaolenga kuleta mabadiliko chanya kwa jamii badala ya kuendeshwa na siasa, ambazo zimekuwa zikikumba baadhi ya vikundi hivyo.

“Ninatamani muweke mkazo katika kutoa elimu itakayowawezesha viongozi wa BMU kusimamia ipasavyo rasilimali za bahari pamoja na mapato na matumizi yake, ili kuondoa migogoro na vurugu zinazojitokeza hasa wakati wa uchaguzi wa viongozi,” alisisitiza Mangosongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la WATONET, Ndugu Liberatus Mokoki, alitoa wito kwa viongozi wa Serikali, taasisi, wadau wa maendeleo na wananchi kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha Kisiwa cha Mafia kinakuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza katika uhifadhi wa rasilimali za bahari nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Ndugu Mussa Kitungi, alisema utekelezaji wa mradi huo unaakisi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kujenga uchumi jumuishi unaogusa maisha ya kila mwananchi.

Vilevile alitoa rai kwa mashirika mengine na wawekezaji kujitokeza kuunga mkono jitihada za kukuza uchumi wa buluu, akisisitiza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji katika sekta hiyo.

Viongozi wa vikundi shirikishi na wananchi wamepongeza kuanzishwa kwa mradi huo, wakieleza kuwa utasaidia kutatua changamoto zilizokuwepo kwa muda mrefu.

Mkufunzi wa Masuala ya Uhifadhi wa Jamii (CBM) kutoka DOKICHUNDA, inayosimamia maeneo ya Dongo, Kilindoni, Chunguruma na Ndagoni alieleza, Changamoto kubwa zilizokuwepo ni migogoro ya mara kwa mara na uelewa mdogo wa uendeshaji wa BMU. 

“Kupitia mradi huu, tunaenda kufufua matumaini mapya kwa kuimarisha doria, kuongeza uwazi na kuwa na takwimu sahihi za wadau wote wa uvuvi,”

Mradi huo unafadhiliwa na Blue Ventures na unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la WATONET, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia na Hifadhi ya Bahari Mafia (MIMP).