Home LOCAL TASAF KUANZA KUTEKELEZA MIRADI YAKE INAYOFADHILIWA NA OPEC FUND ZANZIBAR

TASAF KUANZA KUTEKELEZA MIRADI YAKE INAYOFADHILIWA NA OPEC FUND ZANZIBAR

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Shedrack Mziray amesema miradi ya maendeleo ya Jamii inayotekelezwa na Mfuko huo kupitia ufadhili wa fedha zinazotolewa kupitia OPEC Fund itaanza kutekelezwa na Zanzibar katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Fedha za OPEC Fund hutolewa na Mfuko wa nchi zinazozozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC FUND) na lengo la kutoa fedha hizo ni kuwezesha kufanikisha kwa miradi ya kijamii katika maeneo ambayo yanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa huduma hizo muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha mwishoni kwa Desemba 2025 alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya OPEC Fund Mziray amesema kwa sasa wapo katika hatua ya kuomba tena fedha za OPEC kwa ajili ya kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika mikoa mingi zaidi ya ile iliyofikiwa katika awamu ya kwanza na pili ya OPEC.

“Tunafikia kuomba zaidi ya dola za Marekani milioni 100 kama wenzetu wa OPEC watakubali lakini pia tunafahamu Serikali inamahitaji mengi kama ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya SGR hivyo wanaangalia na wenyewe kiasi gani kinaweza kwenda TASAF.

“Na katika OPEC inayokuja tutakwenda Zanzibar katika Visiwa vya Unguja na Pemba ili kufanya maendeleo jumuishi hii ni Jamhuri ya Muungano lazima tufaidi keki ya Taifa wote kwa pamoja,”amesema Mziray alipokuwa akieleza namna ambavyo miradi ya OPEC ilivyokuwa na tija katika mikoa ambayo tayari miradi imetekelezwa.

Akifafanua zaidi amesema mradi mpya wa OPEC ambayo TASAF wanaiomba kwanza wanataka kuongeza idadi ya mikoa kwani walikuwa na mikoa miwili ya Lindi na Mtwara ambapo walifanya kwa miaka 10 baadae wakaongeza mikoa miwili ya Arusha na Njombe ambapo walitekeleza mradi kwa miaka mitano.

Pia wakaongeza mikoa ya Mwanza,Simiyu na Geita hivyo OPEC ikawa inatekelezwa katika mikoa mitano ambako nako wameitekeleza kwa miaka 10

Ile ya mwanzo ya OPEC ilikuwa na thamani ya fedha dola za Marekani Milioni 16 ambayo ilitekelezwa Lindi na Mtwara na Awamu ya pili ya OPEC ilikuwa na dola za Marekani milioni 50 na sasa tunategemea kuomba fedha nyingi zaidi kutoka OPEC ili tufike mikoa mingi zaidi na tunatarajia kuomba dola Milioni 100.”

Kuhusu vigezo vinavyotumika kupeleka mradi kusaidia jamii husika, amesema kigezo kikubwa ambacho TASAF inakitumia ni zile halmashauri ambazo zinaupungufu wa huduma za kijamii na kitakwimu zinaonekana ziko chini zaidi kimaendeleo

“Unaweza ukashangaa OPEC tumeipeleka katika mikoa kama Shinyanga, Geita,Simiyu au Mwanza wakati kuna madini lakini ukweli katika huduma za kijamii mikoa hiyo bado huduma muhimu za kijamii zinahitajika hivyo pamoja na jitihada za Serikali kupeleka maendeleo na sisi TASAF tunawajibika moja kwa moja kutatua changamoto za wananchi kupitia miradi ya OPEC.

Amefafanua Mkoa wa kama Katavi ndio inalima sana lakini ndio mkoa wenye huduma chache za kijamii huku akieleza Mkoa kama Dodoma kwa sasa umekuwa na kasi ya maendeleo kwasababu ya Serikali kuhamia Dodoma lakini kwa Mkoa wa Singida katika OPEC inayokuja utakuwa mmoja wa Mkoa ambao utapewa kipaumbele na TASAF.

“Kwahiyo vigezo vya mradi wa OPEC ni sehemu ambazo zina upungufu wa huduma za jamii,ukisikia stori za huko Simiyu au Maswa,Geita ndani kule yaani kuna habari nyingi ambazo ukiangalia kwa ujumla utaona changamoto

“Kwahiyo mkoa kama Singida lazima utakuwepo katika OPEC inayokuja lakini hatutaenda tena Geita ,Simiyu na Mwanza kwasababu huko tumeshaenda na kwa kweli ukiongea na wabunge wa mikoa hiyo utaona matokeo chanya ambayo yamepatikana

“Kwa mfano Karatu hapa kuna jamii ya Wahadzabe na jamii za wafugaji ambao wako mbali na Mjini zaidi ya kilometa 150 kutoka hapa, na wale kule maisha yao sio unayoyaona hapa Karatu Mjini.

“Tunafahamu bado mahitaji ni makubwa lakini pia tunaishukuru Serikali kwa hatua ambazo inaendelea kuzichukua katika kuboresha maisha ya wananchi hasa kwa kupeleka huduma muhimu za kijamii,”amesema Mziray.

Mwisho