Home LOCAL TARURA YAWAKUMBUSHA. WANANCHI   KUCHUKUA TAHADHARI KIPINDI CHA MVUA

TARURA YAWAKUMBUSHA. WANANCHI   KUCHUKUA TAHADHARI KIPINDI CHA MVUA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dar es Salaam

Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari na kuwa makini katika kipindi cha msimu wa mvua ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kujaa kwa maji katika maeneo ya miundombinu ya barabara.

Rai hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Menejimenti ya Wakala, Mameneja wa Mikoa pamoja na Waratibu wa miradi ya dharura kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Seff amesema ni muhimu wananchi kuzingatia alama zote za usalama barabarani katika matumizi ya barabara na kuepuka kuvuka barabara au madaraja yenye maji mengi.

“Ni vyema wananchi kuchukua tahadhari katika maeneo yao au wanapokuwa safarini, endapo daraja limezidiwa na maji wanapaswa kusubiri hadi yapungue hivyo itakua ni njia bora ya kuepusha ajali na kulinda usalama wa miundombinu nchini,” amesisitiza.

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa mara moja pale panapotokea uharibifu wa miundombinu ya barabara kwenye ofisi za Wilaya, Mikoa au Makao Makuu ya TARURA, ili kuzuia ajali zinazoweza kujitokeza.

Mhandisi Seff ameongeza kuwa kwa maeneo ambayo barabara au daraja limesombwa na maji, wananchi wanapaswa kuwa makini zaidi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.