Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!
Dar es Salaam
Mameneja wa Mikoa wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wametakiwa kulinda usalama wa watumiaji wa barabara na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seif, wakati wa kikao kazi cha Menejimenti na Mameneja wa Mikoa kinachofanyika jijini Dar es Salaam.
“Kikao hiki kimekusudia kujadili mikakati ya utekelezaji wa majukumu ya ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya, hususan katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea nchini. Ni muhimu kuweka tahadhari kwenye maeneo ya miundombinu ya barabara”.
Amesema kikao hicho pia kimelenga kujitathmini na kupanga malengo ya mwaka 2026 kwa kuzingatia weledi, uwajibikaji na ubora wa kazi. “Niwahimize maneneja kufanya usimamizi makini wa fedha za Serikali ili kuakisi thamani ya fedha na kuzingatia ubora wa kazi ili wananchi wapate huduma bora za miundombinu ya barabara.
Hata hivyo, Mhandisi Seff amesisitiza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuchukua hatua za kutatua kero za usafiri na usafirishaji, hususan kwa wananchi wa vijijini. Ameeleza kuwa TARURA inalenga kujenga barabara imara na stahimilivu kwa hali ya hewa ili kuchangia maendeleo endelevu na kuimarisha mtandao thabiti wa barabara za wilaya kwa ustawi jumuishi wa Taifa.
Naye, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha Mhandisi Nicholas Francis amesema kuwa, katika kikao kazi kilichofanyika wataalamu wameweka mikakati ya kujipanga ipasavyo katika kipindi hiki cha msimu wa mvua ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
“Imesisitizwa kuwa ni lazima maeneo yote ya miundominu yapitiwe na kufanyiwa ukaguzi, hususan yale hatarishi ili yasijifunge na endapo kutatokea athari, wananchi wanapaswa kupatiwa njia mbadala ili kuendelea na shughuli zao bila usumbufu”.
Aidha, Mhandisi Francis ametoa wito kwa wazazi hususan katika kipindi cha kufunguliwa kwa shule kuchukua tahadhari na kuhakikisha watoto hawapiti katika maeneo yaliyojaa maji na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa kusubiri maji yapite na kama hawana uhakika na usalama wa daraja au kalavati ni vyema wakasubiri pia kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji au ofisi za Wakala.
















