Home LOCAL MSAJILI WA HAZINA AOMBA USHIRIKANO WA PIC KUIMARISHA MAGEUZI YA UWEKEZAJI WA...

MSAJILI WA HAZINA AOMBA USHIRIKANO WA PIC KUIMARISHA MAGEUZI YA UWEKEZAJI WA UMMA

Dodoma. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) leo, Januari 15, 2026 imeendesha semina maalumu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) katika Ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma.
Semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa Bunge wa kuzijengea uelewa mpana kamati zake, ili kuziwezesha kutekeleza majukumu ya kibunge kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Semina hiyo imelenga kuijengea Kamati ya PIC uelewa wa kina kuhusu muundo, majukumu na mwelekeo wa kimkakati wa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali, sambamba na uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa miaka 25 (2026–2050).
Kupitia utaratibu huu wa Bunge, Kamati hupata fursa ya kuelewa kwa undani majukumu, changamoto na mipango ya taasisi wanazosimamia, jambo linalosaidia kuimarisha ubora wa maamuzi, usimamizi na ushauri wa kibunge.
Katika mawasilisho yake, OMH imeeleza historia ya kuanzishwa kwake tangu mwaka 1959, msingi wake wa kisheria chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura ya 370, pamoja na mageuzi ya kimuundo na kisheria yaliyofanyika ili kuiwezesha Ofisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika mazingira ya sasa ya kiuchumi, kibiashara na kiutawala.
 Kamati imeelezwa kuwa OMH inatekeleza majukumu yake makuu katika maeneo manne ya msingi ambayo ni kumiliki na kuhifadhi mali za Serikali kwa niaba ya umma, kuishauri Serikali kuhusu uwekezaji na usimamizi wa mashirika ya umma, kusimamia utendaji kazi wa taasisi na mashirika hayo, pamoja na kusimamia urekebishaji na ubinafsishaji pale inapohitajika.
Aidha, ilisisitizwa kuwa jukumu la msingi la Ofisi ni kuhakikisha mashirika ya umma yanachangia kikamilifu katika Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia mapato yasiyo ya kodi, sambamba na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Katika muktadha huo, Kamati ya PIC imeelezwa kuhusu muundo mpya wa OMH ulioboreshwa mwaka 2023 unaojumuisha Kurugenzi tisa na Vitengo vitano, muundo unaolenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuendana na ongezeko la idadi ya mashirika ya umma pamoja na mabadiliko ya kiteknolojia na kiuchumi.
Sehemu muhimu ya semina hiyo ilikuwa ni uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa OMH kwa kipindi cha 2026 hadi 2050. Kupitia mpango huo, OMH imebainisha dhamira ya kuongoza mageuzi ya kiuchumi kwa kusimamia uwekezaji wa Serikali kwa mtazamo wa muda mrefu, unaozingatia tija, uwajibikaji na uendelevu, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ametoa wito kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na wa dhati kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kusimamia na kuongoza mageuzi ya muda mrefu ya uwekezaji wa umma.
Ameeleza kuwa mafanikio ya Mpango Elekezi wa Muda Mrefu na mageuzi yanayolengwa hayawezi kupatikana bila usimamizi madhubuti, mwongozo wa kisera na uungwaji mkono wa Bunge kupitia Kamati husika.
Bw. Mchechu amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuoanisha mifumo ya kisheria na kitaasisi, kuimarisha utawala bora katika bodi na menejimenti za mashirika ya umma, pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayoiwezesha OMH kusimamia uwekezaji wa Serikali kwa misingi ya kibiashara, uwajibikaji na ushindani.
 Aidha, amebainisha kuwa Kamati ya PIC ina nafasi ya kipekee ya kuhakikisha mageuzi haya yanapata mwendelezo na uthabiti kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina ametoa ahadi kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuwa ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu, taarifa kwa wakati na ushauri wa kitaalamu ili kuiwezesha Kamati kutekeleza majukumu yake ya kibunge kwa ufanisi.
 Ameahidi kuwa OMH itaendelea kuwa wazi, tayari kushirikiana na Kamati katika masuala ya ufuatiliaji, tathmini na usimamizi wa uwekezaji wa umma, pamoja na kutoa ufafanuzi na taarifa zote muhimu zitakazohitajika katika utekelezaji wa majukumu ya kibunge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Masanja Kadogosa, alieleza matarajio yake ya kuona utekelezaji thabiti wa majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) unaoleta matokeo yanayopimika, hususan katika kuimarisha utendaji wa mashirika ya umma, kuongeza mapato yasiyo ya kodi, na kupunguza utegemezi wa mashirika hayo kwenye ruzuku ya Serikali.
Ujumbe mkuu kutoka kwa Bw. Kadogosa, pamoja na wajumbe wengine wa kamati, ni wito kwa mashirika ya umma kuzalisha kwa tija ili kuchangia katika pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi
“Tunatarajia kuona uwazi, utawala bora na uwajibikaji katika usimamizi wa uwekezaji wa umma,” alisisitiza, huku akisema, “sisi kama kamati, tupo tayari kuisaidia Ofisi ya Msajili wa Hazina kutekeleza mageuzi katika mashirika ya umma.”