
● Asisitiza: Hati za nyumba na dhamana za watumishi wa Serikali hazihitajiki
● Asema: Vitambulisho vya NIDA vinatosha
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameyataka Majiji na Halmashauri wahakikishe masharti magumu kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 yanaondolewa ili kuwapa fursa wananchi wengi zaidi kupata mikopo hiyo.
Dkt. Mwigulu amesema wananchi wanaweza kutumia vitambulisho vya Taifa (NIDA). Wale wasio na vitambulisho vya Taifa wanaweza kutumia barua za utambulisho kutoka ofisi za Serikali za Mitaa au Vijiji.
Amesema hayo leo Alhamisi, Januari 29, 2026, bungeni jijini Dodoma, akijibu swali la Mheshimiwa Agnesta Kaiza, Mbunge wa Segerea, kuhusu mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa mikopo hiyo hutolewa kwa makundi maalum: wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4), na wenye ulemavu (asilimia 2), ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi. “Hakuna haja ya masharti magumu,” alisema.
Aidha, Dkt. Mwigulu alisema kuwa ndani ya kipindi cha siku 100, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha ongezeko la shilingi bilioni 200 katika mfuko wa mikopo ili kuongeza wigo wa mikopo kwa wananchi wote.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anamaanisha katika suala la kuwawezesha vijana, wanawake, na ndugu zetu kutoka makundi maalum. Ndiyo maana kaongeza Shilingi Bilioni 200 katika siku 100 baada ya kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa hatua hizi ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, na kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii.
Akijibu swali la Mheshimiwa Esther Maleko, Mbunge wa Viti Maalum, Waziri Mkuu alisema:
“Ninatoa wito kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuzingatia miongozo iliyopo, hasa ya uvunaji wa miti katika mashamba, badala ya kuvuna miti asili ambayo kukua kwake ni kwa muda mrefu.”
Akijibu swali la Dkt. Ritha Kabati, Mbunge wa Kilolo, kuhusu huduma ya Bima ya Afya kwa wote, Waziri Mkuu alisema:
“Kujiunga na Bima ya Afya kwa wote ni jambo la msingi kwa Watanzania, kwa sababu itawezesha kumudu gharama za matibabu. Sisi upande wa Serikali tutaendelea kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa uhakika.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 29, 2026




