Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!
– asema motisha ni nguzo ya huduma bora kwa wananchi
Na. Mwandishi wetu,
NAMTUMBO.
Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Dkt. Juma Zuberi Homera, ameendelea kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuwajengea motisha na mazingira bora ya kazi watumishi wapya, baada ya kukabidhi magodoro 222 kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, hatua inayolenga kuinua morali na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Magodoro hayo yamegawanywa kwa mpangilio mahsusi ambapo 202 kwa watumishi walioajiriwa tayari, 13 kwa watumishi wanaotarajiwa kuajiriwa, na 7 kama akiba.
Makabidhiano yamefanyika tarehe 23 Januari 2026 katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali na Chama, Dkt. Homera amesema motisha kwa watumishi si hisani bali ni mkakati wa maendeleo, akisisitiza kuwa ajira mpya na ustawi wa watumishi vinaenda sambamba na ubora wa huduma kwa wananchi.
“Tunapoweka mazingira rafiki ya kazi, tunajenga Taifa lenye tija,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya utumishi wa umma, hususan utekelezaji wa ajira mpya na kuboresha huduma ndani ya kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais Samia.
Aidha, amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo, huku akiomba viongozi kuweka mazingira wezeshi ikiwemo upatikanaji wa maeneo ya kilimo kwa ustawi wao.
Kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Francis Pili, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Musa Mumina, wamempongeza Dkt. Homera wakisema motisha hiyo ni ya kwanza na ya mfano, itakayochochea morali na uwajibikaji kazini.
Nao watumishi waliopokea msaada huo wamesema kitendo hicho kimewapa hamasa mpya, wakiahidi huduma bora, nidhamu na kujituma kwa maslahi ya wananchi wa Namtumbo.







