

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo,akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC, alipofanya ziara kwenye Ofisi za Shirika hilo Makao Mkuu, leo January 5, 2026, Jijini Dar es Salaam,
-Usimamizi wa ujenzi unavyosumbua wananchi
– Asema NHC inaweza kuwaondolea wananchi tabu hiyo
– Awataka watendaji wasiwe maafisa mchakato
Mwandishi Wetu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, amefanya ziara makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC), na kuliagiza kufanya tafiti kisha kuja na jawabu la upatikanaji wa nyumba bora za kisasa kwa watanzania wa kawaida.
Dkt. Akwilapo ametoa agizo hilo katika ziara yake lalipotembelea Ofisi za NHC Makao makuu, leo Januari 5, 2026 Jijini Dar es Salam, ambapo amekutana na menejimenti, kisha kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika hilo.
Katika hotuna yake, Dkt. Akwilapo, ametumia nafasi hiyo kujitambulisha ikiwa ni mara yake ya kwanza kutembelea Shiririka hilo, tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Fanyeni tafiti za nyumba za gharama nafuu kwa watanzania wa kawaida. Nawatuma mjenge nyumba bora za bei nafuu kwa ajili ya watanzania wenye kipato cha kawaida, kwani Watanzania wanaingalia NHC,” amesema.
Aidha, amewataka watumishi wa NHC kufanya kazi kwa kuheshimiana na kuheshimu wananchi wanaofika kwenye ofisi za shirika hilo kufuata huduma, zikiwemo taarifa mbalimbali za makazi na umiliki wa nyumba.
Pia amesema kuwa NHC ina dhima kubwa ya kuhakikisha hata wananchi wa kawaida wanapata nyumba bora, akisisitiza kufanya utafiti utakaokuwa mwarobaini wa tatizo hilo.
Amewaonya watumishi hao kwa kuwataka wasiwe maofisa wakufanya michakato, ambao kila wanapokutana na wateja wanawaeleza jambo husika bado lipo kwenye mchakato.
Vilevile Dk. Akwilapo pia ameiagiza NHC kuendelea na kasi ya utekelezaji wa miradi yake, na kuepuka ucheleweshaji ili kukwepa kuongeza gharama katika miradi hiyo.
“Shirika liongeze kasi ya kukusanya madeni ya wateja wake, ili fedha ziliwezeshe NHC kufikia malengo yake,” ameagiza Dk. Akwilapo.
“Matarajio yangu ifikapo mwaka 2030, NHC inafikia malengo yake katika kutekeleza malengo ya Wizara na Serikali kama yanavyoongozwa na Ilani ya chama tawala, CCM.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema shirika lake linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara nchini.
Amesema katika utekelezaji wake, kwa mwaka 2025 NHC ilipata tuzo tatu tofauti kutokana na utendaji wake kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo gawio kwa Serikali.
“Mwaka uliopita NHC ilipata mafanikio mbalimbali, ikiwemo tuzo tatu kutokana na utendaji bora kwenye maeneo tofauti,” amesema Hamad.
Amesema NHC kwa mwaka 2026 itajikita katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya makazi na biashara ikitambua dhima iliyonayo ya kutekeleza ajenda ya Serikali ya makazi bora, salama na nafuu kwa watanzania.


Awali, akimkaribisha Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri wa wizara hiyo Caspar Mmuya, amewahimiza watumishi wa NHC kutoishia kuhudumia wananchi kwa kuwapatia nyumba bora, bali nao wawe wamiliki wa nyumba bora kwa ajili ya familia zao.
Meneja Habari na Uhusiano wa NHC Muungano Saguya, akizungumza alipokuwa akitoa salamu za ukaribisho mapema wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, alipotembelea makao makuu ya Shirika hilo, leo January 5,2026, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Rasilimali watu wa NHC, Bi. Fatuma Chillo, akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Shirika hilo, katika ziara hiyo.







