
Na; OWM (KAM) – DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa hatua kubwa ilizochukua katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, hususan utoaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaokumbana na madhila ya ajali ama ugonjwa unaotokana na kazi.
Mhe. Waziri ametoa pongezi hizo Desemba 10, 2025 Jijini Dodoma wakati wa ziara yake katika Ofisi za Makao Makuu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) alipokutana na Menejimenti na baadhi ya watumishi wa WCF kwa lengo la kujua majukumu ya Mfuko huo sambamba na kutoa maelekezo ya kiutendaji yanayolenga kuongeza tija na ufanisi kuendana na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Mhe. Sangu amesema huduma hizo bora zimechangia kuimarisha imani ya wananchi kwa Mfuko, ambapo wafanyakazi wanaopatwa na majanga kutokana na kazi wamekuwa wakipatiwa huduma kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili, jambo ambalo limeongeza ufanisi na kupunguza usumbufu kwa wafanyakazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameitaka Menejimenti ya WCF kuendeleza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kuongeza nguvu ya mifumo mipya ya kidijitali inayoboresha mbinu za utoaji huduma kwa wakati na ufanisi na kufikia wananchi kwa haraka zaidi.
Awali, akizungumza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, amehamasisha Menejimenti ya Mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na Mfuko, ili kuongeza uelewa kwa waajiri wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema WCF imejipanga kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha madai ya fidia yanashughulikiwa kwa wakati, uwazi na ufanisi zaidi.
Mwisho.





