
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini Mhe Anthony Peter Mavunde, amempongeza Afisa madini mkazi (RMO) wa mkoa wa kimadini wa Mirerani, George Kaseza kwa namna anavyotekeleza wajibu wake ipasavyo, bila kulalamikiwa au kubagua wachimbaji.
Waziri Mavunde ameeleza hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, alipofanya ziara ya kutembelea machimbo ya madini ya Tomarini ya kijani eneo la Lemshuku na madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.
Amesema RMO Kaseza ni kiongozi mzoefu katika suala zima la eneo tengefu la Mirerani ndiyo sababu akateuliwa kuwa kiongozi wa hapo ambaye wadau wa madini pia wanamkubali kupitia utendaji kazi wake.
“RMO Kaseza umekuwa mara nyingi ukiandika maandiko mengi ya eneo tengefu la Mirerani ndiyo sababu tukakuleta hapa sasa yake maandiko yako yafanye kuwa uhalisia ili yaonekane kwa vitendo,” amesema Waziri Mavunde.
Amewaasa wadau wa madini wa eneo hilo kumpa ushirikiano wa kutosha RMO Kaseza ili aweze kuwatumikia na pia kufanya vyema kazi yake ya uongozi kupitia nafasi hiyo aliyonayo.
“Waswahili wanasema mchawi mpe mtoto amlee ndiyo sababu RMO Kaseza akateuliwa kuongoza eneo hilo la Mirerani, kutokana na ufahamu alionao na uzoefu wake,” amesema Waziri Mavunde.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amempongeza RMO Kaseza kwa kuwatumikia ipasavyo wana Mirerani kwa weledi.
“RMO Kaseza ni kiongozi ambaye ni msikivu na kunapokuwa na changamoto za wachimbaji tunazifikisha ofisini kwake na zinafanyiwa kazi bila tatizo,” amesema Elisha.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wanawake nchini (TAWOMA) Rachel Njau amesema RMO Kaseza ni kiongozi ambaye akiwasilishiwa changamoto anashirikiana na wenzake katika kuzitatua.
Makamu Mwenyekiti huyo wa TAWOMA ameeleza kwamba hata changamoto za wanawake wauza magonga zimefanyiwa kazi na RMO Kaseza mara baada ya kufikishwa ofisini kwake.




