
Leo tarehe 19 Desemba, 2025, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo kwa pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Palamagamba Kabudi walikutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi Mheshimiwa Sergey Victorovich Lavrov. Kikao hicho kimefanyika tarehe 19 Desemba, 2025, Cairo, Misri pembezoni mwa Mkutano wa Jukwaa la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Urusi na Nchi za Afrika, unaoendelea nchini Misri.
Katika mazungumzo yao Mawaziri hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi kupitia biashara, na uwekezaji. Nchi hizo pia zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati ikiwemo Elimu, Nishati, Afya, Kilimo, Miundombinu, Uchukuzi, na Utalii.
Pamoja na mahusano mazuri yanayoendelea kati ya Urusi na Tanzania, Mheshimiwa Waziri Kombo amemthibitishia Mheshimiwa Waziri Lavrov utayari wake katika kushirikiana na Serikali ya Urusi katika kuwezesha na kufanikisha utekelezaji wa miradi na masuala mbalimbali ya ushirikiano. Aidha, kwa upande wake Mheshimiwa Waziri Lavrov ameahidi kuipatia Tanzania ushirikiano utakaohitajika katika maeneo yanayokusudiwa ili kuendelea kudumisha uhusiano wa kihistoria wenye maslahi mapana baina ya Tanzania na Urusi.





