
MKURUGENZI wa Halmashauri ya jiji la Dar-es Salaam, Elihuruma Maberya, amewataka watendaji na watumishi wa halmashauri hiyo kuchapa kazi kwa kuhakikisha wanasaidia Serikali kukusanya mapato.
Huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amewataka madiwani na watumishi wa jiji hilo wakasimamie mapato ya Serikali pamoja na miradi ya maendeleo.
Maberya, amezungumza hayo katika ufunguzi wa Baraza la Madiwani wa halmashuri hiyo ambapo amesema katika mwaka wa fedha uliopita Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam ilifanya vizuri katika mapato.
“Tumefikia bajeti shilingi bilioni 132, nawaomba watendaji wangu na watumishi tufanye kazi kwa weledi katika kukusanya mapato na kutatua kero za wananchi,tumsaidie Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ili nchi yetu iweze kukua kiuchumi,” amesema Maberya.
Pia amesema, katika uongozi uliopita uliweza kusimamia na kukamilisha miradi yote ya maendeleo pamoja na kuwaondoa wakandarasi wazembe ambapo katika miradi hiyo baadhi yake ikiwemo vituo vya afya Mchikichini na Mzinga ambacho kinatarajiwa kumalizika hivi karibuni.
Sanjari na hayo amesema,bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fiedha 2025 /2026 ni bilioni 152, ambayo yote inakwenda katika miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam Nurudin Juma (Shetta), amesema atakwenda kusimamia maslahi ya madiwani wake, mapato ya Halmashauri hiyo, miradi ya maendeleo pamoja na kutekeleza Ilani ya chama vizuri.






