
Na Mwandishi Wetu
Shilingi bilioni 16 zinatarajiwa kutumika katika kipindi cha miaka minne kutekeleza Mradi wa Baridi Sokoni, unaotekelezwa katika vijiji 60, wilaya sita na mikoa minne.
Mradi huo unatekelezwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa ufadhili kutoka Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Chakula na Kilimo (GAFSP), na unasimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mradi unatarajiwa kuwafikia wakulima 4,000 wanaojihusisha na kilimo ikolojia cha viungo na mboga mboga.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Katibu wa Mradi wa Baridi Sokoni, Asela Kavishe, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Kata ya Kibogwa, Tarafa ya Matombo, wilayani Morogoro Vijijini.
Alisema mradi huo ulianza Machi mwaka jana, ukihusisha Mkoa wa Morogoro katika wilaya za Mvomero na Morogoro Vijijini, Mkoa wa Njombe katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Kilimanjaro katika Wilaya ya Same, pamoja na Kaskazini Unguja katika wilaya za Kaskazini A na B.
Kavishe alisema mradi unalenga mazao ya viungo yakiwemo karafuu, pilipili hoho, mdalasini na tangawizi, huku mazao ya mboga yakijumuisha nyanya, njegere, maharage na vitunguu saumu.
“Lengo kuu la mradi ni kuboresha mifumo ya uzalishaji na masoko kwa kilimo ikolojia, ambacho kinazingatia afya ya mazingira, udongo, mimea na walaji, pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Aliongeza kuwa mradi pia unatoa mafunzo kupitia shule za wakulima shambani kwa wakulima wadogo waliopo kwenye mitandao na vikundi, hatua inayoongeza ufanisi katika kilimo ikolojia.
Kavishe alisema mradi umewezesha wakulima kujifunza mbinu sahihi za upandaji, maandalizi ya mashamba, udhibiti wa visumbufu na magonjwa kwa njia za ikolojia, pamoja na utunzaji wa mazao baada ya kuvuna.
Alisema wakulima wamenunua miche bora ya viungo na vitunguu saumu na kuipanda kwa kutumia mbinu sahihi.
“Tulinunua tani sita za vitunguu saumu na kuwagawia wakulima 403, hali iliyowezesha Wilaya ya Mvomero kuwa na zaidi ya wakulima 700 wanaojihusisha na aina hii ya kilimo,” alisema.
Aliongeza kuwa mbegu za nyanya ziligawiwa kwa wakulima 507, jambo linalotarajiwa kuongeza kipato chao katika siku za usoni.
Aidha, alisema mradi unalenga kuhakikisha wakulima wa mazao hayo wanapata masoko makubwa na ya uhakika kutokana na uzalishaji unaozingatia mifumo ya kilimo ikolojia.
Kavishe alisema mradi unasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuwapatia wakulima mafunzo ya kutumia pembejeo zinazopatikana shambani na kuwawezesha kuanzisha vitalu vyao wenyewe.
“Tumeanzisha vitalu 12 vya mdalasini na karafuu vyenye miche 17,500, na matarajio yetu ni kwamba baada ya mvua za masika wakulima wataweza kupanda. Hii itahakikisha upatikanaji wa miche bora ya viungo na kuondoa tabia ya kuchukua miche duni,” alisema.
Alisema uanzishwaji wa vitalu una faida mbili kwa wakulima: kupanda katika mashamba yao na kuuza miche kwa wakulima wengine.
Kutokana na hilo, wanatarajia eneo la kilimo kuongezeka katika siku za usoni.
Kwa upande mwingine, Kavishe alisema mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 16 katika awamu mbili, unapanga kujenga maghala saba katika vijiji vinavyoshiriki.
Alisema pia vikundi vya VICOBA na SACCOS vimeimarishwa, hali itakayowawezesha wakulima kupata mikopo na kuwekeza katika kilimo.
Aliongeza kuwa kupitia Mfuko wa Mzunguko wa Mradi wa Baridi Sokoni, wameweza kununua tani 8.1 za karafuu zenye thamani ya shilingi milioni 151.6 kutoka kwa wakulima 73.
Alisema mfumo huo wa masoko ya pamoja umeongeza uzalishaji na mapato kwa wakulima wa viungo.
“Kwa kweli, kupitia mradi huu tunalenga kuboresha mifumo ya uzalishaji, kuongeza kipato, kuimarisha miundombinu ya kifedha na kuhakikisha masoko ya uhakika,” alisema.
Kavishe pia alisema kuwa MVIWATA kupitia Mradi wa Baridi Sokoni inapanga kujenga kiwanda cha kuchakata viungo katika eneo la Kiroka, Morogoro Vijijini.
Mwenyekiti wa MVIWATA na Mjumbe wa Bodi ya Jukwaa la Wakulima Wadogo Afrika Mashariki na Kusini (ESAFF), Apolo Chamwela, alisema kile kinachofanywa na Baridi Sokoni kinaweza kuleta tija endapo serikali itaweka mazingira rafiki kwa wanunuzi kuwafikia wakulima.
Aliongeza kuwa iwapo serikali itaweka mazingira hayo mazuri, uhamaji wa vijana kutoka vijijini kwenda mijini utapungua kwa kiasi kikubwa.
Wakizungumza kuhusu mradi huo, baadhi ya wakulima walisema unaleta mabadiliko katika kilimo.
Theodor Mkude kutoka Kijiji cha Pinde, Kata ya Pinde, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro, alisema kilimo ikolojia kimeanza kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika familia yake.
Mwanahamisi Rashidi kutoka Kijiji cha Kibogwa, Kata ya Kibogwa, Morogoro Vijijini, alisema mradi huo umemfanya aipende kilimo zaidi kwa kuwa unazingatia masuala muhimu kama maandalizi ya ardhi, mbinu za upandaji na upatikanaji wa masoko.





