http://UKAGUZI WA MABASI YA ABIRIA WAFANYIKA KUDHIBITI AJALI.
Na. Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi.
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Jeshi la Polisi Nchini kupitia kikosi cha Usalama barabarani limefanya ukaguzi maalumu wa mabasi ya abiria kwa ajili ya kudhibiti ajali kutokana na ongezeko kubwa la abiria kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mkuu wa Operesheni Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Joseph Mwakabonga leo wakati akizungumza na madereva katika Stendi kuu ya mabasi Mkoani Arusha, amesema kuelekea mwisho wa mwaka kunajitokeza ajali kwa sababu madereva wengi wanakuwa na mihemko ya kutaka kusafirisha abiria wengi kwa muda mfupi.
ACP Mwakabonga amebainisha kuwa wanaendelea na operesheni hiyo nchi nzima ili kutoa elimu kwa madereva na abiria pamoja na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kama siyo kuisha kabisa.
Aidha, amewataka madereva kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani kwani Jeshi hilo halitakuwa na muhali kwa yoyote atakayebainika kukiuka sheria.
Sambamba na hilo, amewataka madereva kujiepusha kuendesha vyombo vya moto huku wakiwa wamelewa, mwendokasi pamoja kuyapita magari mengine kwa uzembe katika maeneo hatarishi bila kuchukua tahadhari za kiusalama.
Kadhalika, amesisitiza kuwa madereva watakaobainika kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani.
Naye Bw. Issa Mohamed ambaye ni dereva wa basi la abiria pamoja na kushukuru kwa elimu waliyoipata, amesema ataenda kuwa balozi mzuri kwa madereva wenzake kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara ya ajali ambayo yanaweza kutokea.
Naibu Mkugenzi wa Elimu na Operesheni wa Shirika la kutetea haki za Abiria Tanzania (SHIKUHA) Bw. Godwin Mpinga amebainisha kuwa changamoto inayowakabili abiria wengi msimu huu ni ongezeko la nauli, hivyo shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa abiria kuhakikisha wanalipa nauli iliyopo kwa mujibu wa sheria lakini pia kuepuka kukatiwa tiketi kwa njia ya karatasi.





