
Klabu ya wekundu wa Msimbazi Simba SC, imetangaza ofa maalum ya punguzo la bei ya jezi zake kuelekea msimu wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, ambapo jezi zote za klabu hiyo sasa zitauzwa kwa shilingi 12,000 badala ya shilingi 45,000 zilizokuwa zikitumika awali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 16, 2025, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema ofa hiyo itadumu kwa siku 45 kuanzia Desemba 16, 2025 hadi Januari 30, 2026.
Ahmed Ally ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuendana na mabadiliko ya soko la kimataifa pamoja na kupambana na tatizo la jezi bandia.
“Tunawataarifu Wanasimba wote waliopo Tanzania na duniani kote kuwa tumetoa punguzo la bei ya jezi kutoka shilingi 45,000 hadi shilingi 12,000. Ofa hii ni ya msimu wa sikukuu na inahusisha jezi zote—za ligi, za kimataifa pamoja na jezi za watoto, ambazo tayari zinapatikana madukani,” amesema Ahmed Ally.
Ameongeza kuwa punguzo hilo pia ni mkakati wa kupambana na jezi bandia sokoni.
“Kama Mwanasimba alikuwa akinunua jezi feki kwa shilingi 15,000, sasa anaweza kupata jezi halisi kwa shilingi 12,000. Uamuzi ni wa Mwanasimba mwenyewe,” ameongeza.
Aidha, Ahmed Ally amewahimiza mashabiki wa klabu hiyo kutumia fursa ya ofa hiyo, hususan kipindi cha sikukuu.
“Ofa hii inaanza leo Desemba 16, 2025 na itaendelea hadi Januari 30, 2026. Kuna Wanasimba wanaosafiri kwenda nyumbani kwa sikukuu, tusikubali kwenda mikono mitupu—nunua jezi za Simba kama zawadi,” amesema.




