Home LOCAL SHIRIKA LA NYUMBA LAMALIZA MWAKA KWA KUMPA FARAJA MLEMAVU WILAYANI SIMANJIRO

SHIRIKA LA NYUMBA LAMALIZA MWAKA KWA KUMPA FARAJA MLEMAVU WILAYANI SIMANJIRO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi Wetu, Mirerani, Manyara

Shirika la Nyumba la Taifa limeumaliza mwaka kwa faraja kwa kuikabidhi Halmashauri ya Wilaya Simanjiro nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 60 iliyoijenga kwa ajili ya kumsaidia mlemavu Ally Juma Marwa mkazi wa Mererani, Mkoani Manyara.

Msaada huo umekabidhiwa Desemba 31, 2026 kwa Afisa Mtendaji wa Mji Mdogo wa Mirerani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri hiyo, na Bw. Muungano Saguya ambaye ni Meneja Habari na Uhusiano wa NHC.

Akikabidhi msaada huo, Bw Saguya amesema kwamba kupitia sera ya Huduma kwa Jamii ya Shirika hilo, NHC ililazimika kumjengea mlemavu huyo kama sehemu ya kurejesha kwa jamii faida inayopata kupitia miradi inayotekelezwa na Shirika hilo katika maeneo mbalimbali nchini. NHC ilishiriki kujenga jengo la Soko la Madini adimu ya Tanzanite lililogharimu shilingi Bilioni 4.5 ambalo limekamilika ili likabidhiwe kwa Halmashauri hiyo wakati wowote kuanzia sasa. Bw Saguya amesema kuwa katika kipindi cha miaka serikali ya Awamu ya sita ya Mheshimiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, NHC imetoa misaada mbalimbali ya kijamii iliyogusa kusaidia miradi ya elimu, afya na walemavu inayogilia shilingi Bilioni 2.41, ambayo imesaidia kuwapa faraja na huduma bora wafaidika.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afisa Mtendaji wa Mji mdogo wa Mirerani Bw. Isaac Mgaya alilishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa msaada huo na amelihakikishia kuwa Halmashauri hiyo itahakikisha miundombinu ya maji na umeme inapelekwa mapema iwezekanavyo katika nyumba hiyo ili iweze kutumika kisha watamkabidhi mhusika.

Akitoa shukrani zake kwa NHC, Bw. Marwa amesema kuwa msaada huo umemrejeshea furaha na matumaini ya kuishi vema na umemuondolea adha ya kudaiwa kodi huku akiwa hana uwezo wa kuilipa kutokana na hali aliyo nayo. Ametaka taasisi zingine ziwasaidie walemavu ili kuwapa faraja na matumaini ya kuishi kama binadamu wengine.