Home LOCAL SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA ULINZI NA MATUNZO KWA WAZEE NA WASIOJIWEZA

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA ULINZI NA MATUNZO KWA WAZEE NA WASIOJIWEZA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Serikali imeendelea kutoa huduma za ulinzi na matunzo kwa wazee na wasiojiweza kwa ufanisi mkubwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali na watoa huduma binafsi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha ustawi wa kundi hilo muhimu katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, Wizara imetoa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi, mavazi, matibabu pamoja na utoaji wa bima ya afya bila malipo kwa wazee zaidi ya 1,256,544, ambao wamepatiwa vitambulisho vya matibabu na bima ya afya bure.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutoa huduma za matunzo kwa wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee 13 yanayomilikiwa na Serikali, ambayo ni Kibirizi (Kigoma), Njoro (Kilimanjaro), Kolandoto (Shinyanga), Bukumbi (Mwanza), Ipuli (Tabora), Fungafunga (Morogoro), Mwanzange, Misufini (Tanga), Nunge (Dar es Salaam), Nyabange (Mara), Kilima (Kagera), Sukamahela (Singida) na Magugu (Manyara).

Kwa mujibu wa Waziri Gwajima, makazi hayo kwa sasa yanawahudumia jumla ya wazee 245, wakiwemo wanaume 147 na wanawake 98. Aidha, Wizara imeendelea kufanya ufuatiliaji wa huduma kwa wazee 279 (wanaume 118 na wanawake 161) waliopo katika Makazi ya Wazee 16 yanayomilikiwa na taasisi binafsi.

Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima amesema Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, Toleo la 2024, ambayo pamoja na mambo mengine imeanzisha Mabaraza ya Wazee kama majukwaa muhimu kwa ajili ya wazee kujadili masuala yao na kutoa maoni pamoja na ushauri katika masuala ya kijamii.

Amebainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2025, jumla ya Mabaraza ya Wazee 20,768, sawa na asilimia 98, yameanzishwa kuanzia ngazi ya Kijiji au Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa hadi Taifa.

“Tunatoa wito kwa jamii kuyatumia mabaraza ya wazee kama chombo muhimu cha kurithisha jamii maarifa, mila na desturi chanya pamoja na maadili mema,” amesema Waziri Gwajima.

Serikali imesisitiza itaendelea kuboresha mifumo na huduma kwa wazee ili kuhakikisha wanapata haki, heshima na maisha bora wanayostahili.