Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Jumuiya za Ukanda wa Maziwa Makuu na Nchi Wanachama wa Mkataba wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Eneo la Maziwa Makuu, uliyofanyika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda.Mkutano huo, umejadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kutafuta amani ya kudumu ya eneo hilo.
Mkutano huo umeongozwa na Rais wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa Kikanda wa Uangalizi wa Mkataba wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Eneo la Maziwa Makuu (Regional Oversight Mechanism for Peace, Security and Cooperation – Framework for the DRC and region) Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma pamoja na Naibu Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli.





