Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), ametangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho, Mhe.Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea leo tarehe 11 Desemba 2025Jijini Dodoma Katika taarifa hiyo, Spika Zungu amesema:
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mhe. Jenista Joakim Mhagama kilichotokea leo 11 Desemba,2025 Jijini Dodoma. Natoa pole kwa Waheshimiwa Wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Peramiho.
Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”Aidha, Ofisi ya Bunge ikishirikiana na familia ya marehemu imesema inaendelea kuandaa mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitatolewa mara zitakapokamilika.
Mhe. Jenista Mhagama, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, amekumbukwa kama kiongozi mahiri, mchapakazi na mwenye kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina,” imehitimisha taarifa hiyo.





