Home LOCAL WAZIRI MKUU MTEULE AAHIDI NIDHAMU, UWAJIBIKAJI

WAZIRI MKUU MTEULE AAHIDI NIDHAMU, UWAJIBIKAJI

Baada ya kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka wazi kwamba safari ya kupambana na umaskini nchini inahitaji nidhamu, uwajibikaji na huduma yenye heshima kwa kila mwananchi katika taasisi za Serikali. Ametoa msimamo mkali dhidi ya watumishi wa umma wazembe, wavivu, wala rushwa na wenye lugha mbovu, akisisitiza kuwa watachukuliwa hatua.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Akiwahutubia Wabunge leo Novemba 13, 2025, Dkt. Nchemba amesema licha ya utajiri wa taifa, bado asilimia 8% ya Watanzania wanaishi katika umaskini wa kupindukia na asilimia 26% wanaishi kwa mlo mmoja. Amesema hana taarifa hizo kwa kuzisoma tu kwenye vitabu, bali kwa kuzishuhudia mwenyewe kupitia maisha aliyokulia kijijini kwa takribani miaka 32.

Mimi umaskini wa Watanzania sijausoma kwenye vitabu, nimeuishi. Mheshimiwa Spika, katika miaka yangu takribani 32 nimepitia maisha ya umaskini, maisha ambayo nilikuwa najifunika nguo aliyokuwa anajifunga shemeji yangu,” amesema.

Ameongeza kuwa safari iliyo mbele inahitaji nguvu ya ziada “Watumishi wa Umma na Watanzania wote lazima twende kwa gia ya kupandia mlima; lazima twende kwa gia ya kupita bahari yenye mawimbi na anga lenye mawingu ili chombo kifike salama. Wote walio wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania tuwe tayari, nitakuja na fyekeo na rato. Maono ya Mheshimiwa Rais lazima yatekelezwe.”

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemthibitisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uthibitisho huo unafuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Waziri huyo wa zamani wa Fedha na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mkoani Singida.

Mwigulu amethibitishwa kwa kura za Ndio 369 kati ya kura 371 zilizopigwa, huku kura za Hapana zikiwa 0 na zilizoharibika zikiwa 2.