
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaanza mkakati mpya wa kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kutumia fedha za ndani kabla ya kuhusisha washirika wa maendeleo, ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kupunguza ucheleweshaji unaotokana na michakato mirefu ya mikopo na misaada kutoka nje ya nchi.
Akizungumza leo Jumanne Novemba 18, 2025 wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha miradi ya maendeleo nchini inatekelezwa kwa wakati, huku serikali ikiweka mbele maslahi ya wananchi.
“Muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita tutaanza kufanya miradi wenyewe, halafu mashirika yatatukuta njiani kisha tutakwenda nao. Tutaanza kwa fedha za ndani, kisha wakimaliza taratibu zao watatukuta tukiendelea,” amekaririwa akisema Rais Samia.
Aidha Rais Samia amewataka Mawaziri na Manaibu Mawaziri walioapishwa kuongeza kasi na uwajibikaji katika majukumu yao, akisisitiza kuwa muda wa kutekeleza ahadi kwa wananchi ni mchache ukilinganisha na ukubwa wa majukumu yaliyoko mbele.
“Mambo ambayo tumeahidi kwa wananchi ni mengi mno lakini muda wa kuyatekeleza ni mchache. Kwa hiyo wale mlioapa leo mjue tuna kazi ya kwenda mbio, tena mbio haswa,” amesisitiza.
Rais Samia pia amekemea utoaji wa taarifa zisizoonesha matokeo halisi, akibainisha kuwa wananchi wanapaswa kuona athari za kazi za serikali katika maisha yao, si kusikia kauli tu.
“Sitaki zile za ‘tunaendelea’ au ‘mchakato uko mbioni’, nataka impact (matokeo) na matokeo hayo yawe kwa wananchi na si ofisini kwako,” aliongeza.
Hafla hiyo ya uapisho imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watendaji wakuu na ndugu wa viongozi walioapishwa, wakitarajiwa kuwa na semina elekezi kesho Jumatano ili kupeana dira na mwelekeo wa serikali katika kuwatumikia wananchi chini ya kaulimbiu yake ya Kazi na utu, tunasonga mbele.




