
-Yawezesha Watanzania kumiliki nyumba za kisasa
– Miradi mkakati kuleta mageuzi ya makazi
– Samia Housing Scheme, Kawe 711 na Ubia Kariakoo inavyoongeza kasi upatikanaji makazi bora nchini, fedha za shirika
– NHC yatumia teknolojia rafiki, mikopo nafuu kuwezesha wananchi kumiliki nyumba
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi yake ya kimkakati, miradi ambayo inalenga kuziwezesha familia nyingi zaidi nchini kumiliki nyumba bora, za kisasa na zenye hadhi. Juhudi hizi zimeonekana kwa uwazi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na nje ya jiji, ambapo miradi ya makazi, biashara na ofisi inajengwa kwa viwango vya kimataifa.
Kupitia mpango kazi wake wa muda mrefu, NHC inaendelea kutekeleza miradi ya ndani ya shirika, miradi ya ubia na miradi iliyotolewa kwa zabuni na Serikali pamoja na taasisi za umma na mashirika mengine. Kati ya miradi iliyopewa kipaumbele katika kipindi hiki ni Samia Housing Scheme Kijichi, Mradi wa Ubia Kariakoo, pamoja na Mradi wa Kawe 711, yote yakiwa Dar es Salaam.
Ni dhahiri kwamba ujenzi wa miradi hii ni sehemu ya utekelezaji wa sera na dira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na endelevu. NHC imesisitiza kwamba miradi yake yote inajengwa kwa kutumia teknolojia za kisasa ambazo hupunguza gharama, kulinda mazingira na kuongeza ustahimilivu wa majengo.


Samia Housing Scheme Kijichi: Makazi bora gharama nafuu
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya shirika, Samia Housing Scheme Kijichi ni moja ya miradi mipya na mikubwa inayotekelezwa kwa kasi. Mhandisi wa Mradi, Julieth Prosper, anafafanua kuwa mradi huo utakuwa na majengo 12 yenye jumla ya nyumba 260.
Mchanganuo wa aina za nyumba katika mradi ni kama ifuatavyo:


- Majengo 5 yakiwa na nyumba za vyumba 3
- Majengo 5 yenye nyumba za vyumba 2
- Majengo 2 yenye nyumba za chumba 1
Nyumba zote zitakuwa na sebule, jiko na miundombinu ya kisasa.
Mhandisi Elias John, msimamizi mkuu wa ujenzi, anaongeza kuwa eneo hilo litakuwa na maegesho 300 ya magari, ambapo kila nyumba itakuwa na nafasi ya moja ya kuegesha. Pia kutakuwepo na jengo maalum lenye maduka na huduma nyingine za kijamii ikiwemo ATM, jambo litakalofanya mradi kuwa sehemu kamili ya makazi.

Ujenzi ulianza Agosti 22, 2025 na unategemewa kukamilika Agosti 22, 2027, kwa gharama ya takribani Shilingi bilioni 41.5.
KASi YA MWITIKIO WA WANANCHI

Kwa upande wa mauzo, Ofisa Mauzo na Masoko Mkuu wa NHC, Daniel Kure, anabainisha kuwa mwitikio wa wananchi ni mkubwa. Tayari kati ya asilimia 15 hadi 20 ya nyumba zimeshauzwa, licha ya mradi kuanza kwa muda mfupi tu.
Kure anasisitiza kuwa wateja wanaoweza kununua nyumba wana taratibu tatu rahisi za malipo:
- Malipo ya fedha taslimu, kuanzia asilimia 10 ya thamani ya nyumba
- Malipo kwa awamu ndani ya miezi 6 hadi miaka miwili
- Mikopo ya nyumba (mortgage) kupitia taasisi zaidi ya 20 za kifedha ambazo NHC ina ushirikiano nazo
Kwa mfano, nyumba ya Sh 220 milioni inaweza kununuliwa kwa kuanza na Sh 22 milioni tu, huku taasisi za kifedha zikifadhili kiasi kilichosalia kwa masharti nafuu.
Bei za nyumba katika mradi huo ni:
- Chumba 1 – Sh 112 milioni
- Vyumba 2 – Sh 220 milioni
- Vyumba 3 – Sh 335 milioni
Kure anatoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo, akisisitiza kuwa eneo la Kijichi si mbali kama wengi wanavyolifikiria.
Njia za kufika ni mbili:
- Kupitia Daraja la Kigamboni – Kibada – Kijichi
- Kupitia Barabara ya Kilwa – Mbagala Misheni, umbali wa kilomita 15 pekee kutoka katikati ya jiji.
Kwa mujibu wa NHC, mradi huu utaongeza thamani ya eneo la Kijichi na kufungua fursa mpya za biashara, ajira na maendeleo ya jamii.
MRADI WA UBIA KARIAKOO: MAPATO YAONGEZEKA KABLA YA MUDA.

Meneja wa Miradi ya Ubia wa NHC, Elizabeth Maro, anaeleza kwamba kuanzia mwaka 2024 NHC imeingia makubaliano ya kutekeleza miradi 21 ya ubia katika eneo la Kariakoo. Kati ya hiyo, miradi mitano ipo hatua za mwisho na mingine mitano imeshapata kibali cha matumizi kamili.
Cha kuvutia ni kwamba miradi hii imeanza kuzalisha mapato ndani ya mwaka mmoja, kinyume na matarajio ya awali yaliyokadiria uingizaji wa mapato baada ya miaka miwili.

Kwa sasa NHC ina miradi 23 inayotekelezwa na zaidi ya maombi 100 ya ubia kutoka kwa wawekezaji.
Makadirio mapya yanaonyesha kuwa miradi hiyo, ikiwa imekamilika kwa asilimia 25 tu, itaingiza zaidi ya Shilingi bilioni 6 kwa mwaka, mara tatu ya makadirio ya awali ya Sh bilioni 2.
Hii inamaanisha kuongezeka kwa mapato ya NHC pamoja na mapato ya Serikali kupitia kodi na gawio, hivyo kuchochea uchumi wa taifa.
MRADI WA KAWE 711: MAJENGO YA GHOROFA 17 YAKARIBIA KUKAMILIKA


Kwa upande wa Mradi wa Kawe 711, Daniel Kure anaeleza kuwa mradi huu mkubwa unahusisha ujenzi wa nyumba 400 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026.
Majengo yana ghorofa 17 na yapo mita 300 tu kutoka baharini. Mauzo yameanza tangu mwaka jana na mwitikio ni mkubwa kutokana na ubora wa majengo na hatua za mwisho za ujenzi zinazoendelea.

Mradi utakuwa na:
- Nyumba za vyumba 2, 3 na 4
- Maduka
- Maeneo ya michezo
- Mabwawa makubwa ya kuogelea
- Benki
- Ukumbi na sehemu za mazoezi
Wananchi wanahimizwa kutembelea eneo la mradi ambako maofisa mauzo wapo tayari kutoa huduma za papo kwa hapo.
FAIDA ZA KIJAMII NA KIUCHUMI ZA MIRADI YA NHC

Miradi ya NHC ina mchango mkubwa kwa uchumi na jamii, ikiwemo:
- Kuongeza ajira kwa vijana
- Kuchochea biashara ndogondogo na za kati
- Kuongeza thamani ya ardhi katika maeneo yanayozunguka miradi
- Kutoa makazi salama na yenye hadhi kwa wananchi
- Kugeuza wapangaji kuwa wamiliki wa makazi
Kwa ujumla, miradi ya NHC inaendelea kuboresha maisha ya wananchi na kuleta taswira mpya ya maendeleo katika miji ya Tanzania.





